1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matatizo ya maji Afrika

Lillian Urio25 Agosti 2005

Bara la Afrika, ambalo linakuwa na matatizo mara kw amara, linakabiliwa na tatizo la ukosefu wa maji, ingawa lina vyanzo vingi vya maji.

https://p.dw.com/p/CHf5

Mito miwili mirefu duniani yanapatikana barani Afrika. Mto Nile una urefu wa kilomita 6,400 na Kongo una urefu wa kilomita 4,370. Lakini pamoja na kuwepo kwa vyanzo hivyo na vingine vingi vya maji, Waafrika wanapata shida ya maji.

Waziri wa Afrika Kusini wa masuala ya maji na misitu, Bi. Buyelwa Sonjica, akizungumza katika mkutano uliofanyika huko Sweden katika kuadhimisha wiki ya maji duniani, amesema ingawa Afrika ina mito mikubwa lakini ina kati ya nchi 21 zinazokabiliwa na matatizo ya ukamwe duniani.

Mto Nile na matawi yake unapitia nchi tisa, nazo ni Misri, Uganda, Sudan, Ethiopia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Tanzania, Rwanda na Burundi. Nao mto Kongo, wa tano kwa urefu duniani kimsingi unapitia nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Jamhuri ya Afrika ya Kati na pia kidogo nchi Zambia, Angola na Cameroon.

Mkutano huo ulihudhuriwa na watu 1,400 wakiwemo wataalamu wa masuala ya maji na wawakilishi wa mashiriki yasio ya kiserekali. Bi. Sonjica alisema katika nchi zenye ukame mito inakuwa na maji kwa kipindi kifupi wakati wa msimu wa mvua, hivyo wanahitaji mabwawa ya kuhifadhi maji kwa wakati wa ukame.

Aliongeza kuwa ni wazi kwamba Afrika inahitaji miundo mbinu katika masuala ya maji. Lakini sio Afrika tu hata katika nchi nyingine zinazoendelea.

Pamoja na hayo Waziri huyo alionya kabla ya mabwawa kujengwa ni lazima mambo mawili yazingatiwe. Kwanza watu watakao hamishwa kutoka kwenye sehemu ambayo litajengwa bwawa ni lazima wapewe fidia na pia wafaidike na kujengwa kwa bwawa hilo. La pili ujenzi wa bwawa usiharibu mazingira ya sehemu hiyo.

Waziri huyo alisema cha kusikitisha ni kwamba nchi nyingi zinazoendelea hazina miundo mbinu ya kutosha ya kuhifadhi maji, hasa katika bara lake la Afrika. Afrika ni bara la mwisho katika masuala ya maendeleo ya kuhifadhi maji.

Alifafanua hilo kwa kutoa mfano, katika bara la Marekani Kaskazini kwa kila mtu kuna hifadhi ya kipimo cha mjao wa maji wa cubic mita 6,150, lakini nchi inyoendelea kama Ethiopia ina hifadhi ya kipimo cha mjao wa maji wa cubic mita 43 tu, kwa kila mtu.

Aliongeza hata nchi yake ya Afrika Kusini, taifa lililoendelea kuliko mataifa mengine ya Afrika, wana hifadhi ya kipimo cha mjao wa maji wa cubic mita 746 kwa kila mtu tu.

Kwa mujibu wa taasisi ya kimataifa ya masuala ya maji, yenye makao makuu mjini Stockholm, asilimia 36 tu ya watu wa bara la Afrika wanapata hudumu za kimsingi za maji na taka na takriban watu milioni 288 hawapati maji safi ya kunywa. Hivyo bara hilo linakabiliwa na tatizo kubwa la kutimiza malengo ya mailenia, yaliopangwa na Umoja wa Mataifa.

Kuna Malengo nane ya mailenia na baadhi ya malengo ni kupunguza umaskini duniani kwa nusu, elimu ya msingi kwa wote, kupunguza vifo vya watoto wadogo kwa theluthi mbili, kupunguza vifo vya wazazi kwa robo tatu, kuongeza usawa wa kijinsia, kupunguza kusambaa kwa magonjwa ya UKIMWI, Malaria na mengine, kuhifadhi mazingira, watu kupata maji safi ya kunwya na ushirikiano kati ya nchi tajiri na maskini katika masuala ya maendeleo.

Viongozi wa nchi za dunia waliahidi kujaribu kutimiza malengo haya ifikapo mwaka 2015, katika mkutano mkuu uliofanyika mwezi Septemba mwaka 2000.

Katika harakati za kujaribu kutimiza malengo hayo kuna mpango mpya wa Mawaziri wa Afrika wa masuala ya maji na usafi, kwa kifupi AMIWASH, wakishirikiana na Baraza linalosimamia masuala ya maji na taka la Shirika la Afya duniani.

Waziri Sonjica aliwambia waliohudhuria mkutano huo kwamba Afrika ina uwezo mkubwa wa kutengeneza umeme kutumia nguvu za maji. Mto Kongo unaweza kutengeneza umeme kwa ajili ya Katikati na Kusini mwa Afrika.