1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia yageuza mkondo wa mto Nile kuzalisha umeme

29 Mei 2013

Ethiopia imeanza kutengeneza mkondo mpya wa maji ya mto Nile na kuyaelekeza maji hayo kwenye bwawa kubwa la umeme. Hatua hiyo imezipa wasiwasi Sudan na Misri ambazo zinategemea maji ya mto huo kwa shughuli zao kiuchumi.

https://p.dw.com/p/18g0U
Waziri Mkuu wa Ethiopa Haile Mariam Desalegne
Waziri Mkuu wa Ethiopa Haile Mariam DesalegnePicha: CC-BY-SA- World Economic Forum

Shughuli za kuchimba njia mpya ya maji ya mto nile zilianza rasmi jana. Ethiopia inataka kuyatumia maji hayo katika mradi wa umeme unaotumia nguvu za maji, ambao utagharimu dola bilioni 4.7, na ukikamilika utakuwa ndio mradi wa aina hiyo mkubwa zaidi barani Afrika.

Tayari, mradi huo ambao unajengwa katika mkoa wa Benishangul-Gumuz karibu na mpaka wa Sudan umekwishakamilika kwa asilimia 21. Ukikamilika utakuwa na uwezo wa kutoa megawati 6000 za umeme, kiwango ambacho serikali ya Ethiopia inasema ni sawa na kinachoweza kutolewa na vinu sita vya nyuklia.

Blue Nile, mto ambao Ethiopia imeanza kuugeuzia njia
Blue Nile, mto ambao Ethiopia imeanza kuugeuzia njiaPicha: CC/Lourdes Cardenal

Manufaa ya kikanda

Radio ya taifa ya nchi hiyo ilimnukuu naibu waziri mkuu Demeke Mekonnin, akiwaambia maafisa waliohudhuria uzinduzi wa njia mpya ya maji ya mto Nile, kwamba umeme utakaozalishwa katika bwawa hilo, utazinufasha pia nchi jirani.

Lakini sio kila nchi jirani wa Ethiopia imeshangilia mradi huo. Sudan na Misri zimelalamika, zikidai kubadilisha njia ya maji ya mto Nile kunakiuka makubaliano ya enzi za ukoloni, ambayo yaliipa Misri haki ya kudhibiti asilimia 70 ya maji ya mto Nile. Misri inasema kuwa haina chanzo chochote cha maji kwa watu wake wapatao milioni 90. Watu wa Misri hutegemea mto nile kwa maji ya kunywa, na ya kutumia katika shughuli za kilimo.

Misri yasubiri ripoti ya wataalamu

Mapema wiki hii, rais wa Misri Mohammed Morsi alikuwa nchini Ethiopia, akiambatana na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry, na msemaji wake alikiambia kituo cha televisheni cha Al-Jazeera, kwamba bado wanasubiri ripoti juu ya athari za kuyageuza mkondo wa maji ya mto Nile.

''Tunataka kujua kitakachotokea baada ya kuugeuza mkondo wa maji. Je itachukua miaka 3 au mitano kulijaza bwawa maji? Ikiwa hivyo, hali hiyo itaamua namna nchi Kama Misri na Sudan zitakavyoathirika.'' Alisema msemaji huyo.

Hata hivyo, mkurugenzi mkuu wa shirika la umeme la ethiopia Mihret Debebe, alisema wanachofanya ni kuyatafutia maji ya mto huo njia nyingine kwa mita kadhaa, kuruhusu ujenzi wa bwawa lenyewe, ambalo linajengwa katikati ya mto, ili kurahisisha utendaji kazi. Baadaye maji hayo yatarudishwa katika mkondo wake wa kawaida, alisema Debebe.

Mto Nile una umuhimu wa kipekee kwa Misri
Mto Nile una umuhimu wa kipekee kwa MisriPicha: imago/OceanPhoto

Hakuna haja ya kuogopa

Naye waziri wa nishati wa nchi hiyo Alemayehu Tegenu, ametuliza hofu za nchi jirani, akisema mradi huo unatoa nafasi ya nchi zote ambako mto huo unapitia, kutumia kwa usawa raslimali ya majii yake.

Waziri wa maji wa Misri Bahaa el-Dini amesema nchi yake haipingi mradi huo wa Ethiopia, ikiwa hautakuwa na madhara kwa nchi nyingine. Hata hivyo alisisitiza kwamba malalamiko ya wakulima wa Misri yanayosababishwa na kupungua kwa maji yanayotumika katika kilimo cha umwagiliaji, yanahalalisha azma yao ya kutoruhusu kupotea kwa tone hata moja la maji yanayotiririka katika mto Nile kuelekea kwao.

Mnamo wiki chache zijazo, tume ya wataalamu kutoka Ethiopia, Misri na Sudan inategemewa kutoa ripoti yake juu ya atahari za bwawa hilo la Ethiopia juu ya kiwango cha maji ya mto Nile.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/APE

Mhariri:Hamidou Oummilkheir