1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel azitolea wito nchi za Magharibi kuhusu Urusi

17 Novemba 2014

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel ametoa wito kwa mataifa ya Magharibi kutopoteza matumaini katika kile kinachoonekana kuwa mapambano ya muda mrefu na Urusi kuhusu Ukraine, lakini ameapa kwamba Urusi haitoshinda.

https://p.dw.com/p/1DoYP
Kansela Angela Merkel
Kansela Angela MerkelPicha: picture-alliance/epa/P. Miller

Kauli hiyo ameitoa baada ya viongozi wa kundi la nchi zenye nguvu kubwa za kiuchumi na zile zinazoinukia -G20, kuitumia fursa ya mkutano wa kilele wa G20, kuishutumu vikali Urusi kuhusu uwepo wake Ukraine.

Akizungumza leo akiwa Sydney, baada ya kuhudhuria mkutano wa kilele wa G20 mjini Brisbane, Merkel amesema Urusi imekuwa ikitumia ushawishi wake kudhoofisha usalama wa Mashariki mwa Ukraine, tangu Crimea ilivyojitenga na Ukraine na kujiunga na Urusi.

''Nani angefikiria kwamba miaka 25 baada ya kuanguka kwa Ukuta wa Berlin, baada ya kumalizika kwa vita baridi, baada ya kugawanyika kwa Ulaya na baada ya kumalizika kwa vita vya dunia, kwamba kitu kama hiki kingeweza kutokea katikakati ya Ulaya,'' aliuliza Kansela Merkel.

Merkel ambaye alifanya mazungumzo na Rais Vladmir Putin wa Urusi pembezoni mwa mkutano wa G20 mjini Brisbane, amesema mataifa ya Magharibi yanafanya kila jitihada kwa lengo la kupatikana suluhisho la kidiplomasia katika mzozo wa Ukraine, lakini pia wanazingatia vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Urusi.

Viongozi wa mataifa ya Magharibi akiwemo, Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron na Rais Barack Obama wa Marekani, wamemkosoa vikali Rais Putin kutokana na hatua yake ya kuchochea mzozo wa Ukraine kwa kuwaunga mkono waasi, shutuma ambazo Urusi imezikanusha.

Putin anaonekana kutotishwa

Hata hivyo, Rais Putin anaonekana kutotishwa na ukosoaji huo na vitisho kutoka kwa viongozi wa mataifa ya Magharibi na anaonekana kuendeleza mapambano hata baada ya mkutano wa kilele wa G20. Hadi wakati huu vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Ulaya, havijaleta mabadiliko yoyote ya kisiasa katika eneo la mashariki mwa Ukraine.

Viongozi wa G20 wakiwa katika picha ya pamoja mjini Brisbane
Viongozi wa G20 wakiwa katika picha ya pamoja mjini BrisbanePicha: Andrew Taylor/G20 Australia via Getty Images

Rais Putin alikuwa ni kiongozi wa kwanza kuondoka katika mkutano huo wa G20, wakati viongozi wenzake wakijitayarisha kuzindua mpango wa kuimarisha uchumi duniani. Viongozi hao walikubaliana kuzifanyia mageuzi hatua za kuimarisha uchumi duniani, huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon akiwataka washiriki kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi.

Wakati huo huo, mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kukutana leo mjini Brussels, huku wakiwa katika shinikizo kubwa la kuiwekea Urusi vikwazo vipya baada ya kumalizika kwa mkutano wa G20 na kuhakikisha inafanikisha mpango wa amani.

Wachambuzi wanasema kuwa vitisho vya mataifa ya Magharibi na hatua ya Putin kuondoka mapema kwenye mkutano huo ni dalili ambayo haionyeshi matumaini yoyote ya kutatuliwa kwa mzozo wa Ukraine. Hapo jana (16.11.2014), Rais Petro Poroshenko wa Ukraine, alisema nchi yake imejiandaa kikamilifu kwa vita.

Kauli hiyo ameitoa wakati ambapo mapigano yanaendelea kwenye eneo la Donetsk, na maafisa wa Ukraine wamesema leo kuwa wanajeshi sita wa nchi hiyo na askari polisi watatu, wameuawa mashariki mwa Ukraine katika muda wa saa 24 zilizopita.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/ AFPE,DW
Mhariri:Yusuf Saumu