1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trilioni za dola zalengwa katika ukuajii mpya wa uchumi duniani

16 Novemba 2014

Viongozi wa kundi la G20 la nchi zenye nguvu kubwa za kiuchumi duniani Jumapili (16.11.2014) wamejitolea kuzifanyia mageuzi hatua za kukuza uchumi kwa asilimia 2.1 kufikia mwaka 2018.

https://p.dw.com/p/1DoMh
Rais Barack Obama(kulia) Waziri Mkuu wa Australia Tony Abbott (katikati) na Waziri Mkuu wa Japani Shinzo Abe(kulia) katika mkutano wa G20 mjini Brisbane. (16.11.2014)
Rais Barack Obama(kulia) Waziri Mkuu wa Australia Tony Abbott (katikati) na Waziri Mkuu wa Japani Shinzo Abe(kulia) katika mkutano wa G20 mjini Brisbane. (16.11.2014)Picha: Reuters

Ahadi hiyo inayojulikana kama "Mpango wa Utekelezaji wa Brisbane" utaongeza ukuaji wao wa uchumi wa pamoja kupindukia asilimia mbili ambayo walikuwa wameilenga awali katika juhudi za kuimarisha uchumi wa dunia unaozorota na kuzalisha ajira.

Viongozi akiwemo Rais Barack Obama wa Marekani na Rais Xi Jinping wa China wamesema katika azimio la mkutano huo wa kilele baada ya mazungumzo ya mwishoni mwa juma kwamba "Zaidi ya trilioni mbili zitaongezwa kwenye uchumi huo wa dunia na kuanzisha mamilioni ya ajira."

Taarifa ya azimio hilo pia imekubaliana juu ya mpango wa dunia kushughulikia pengo la dola trilioni 70 zinazohitajika katika miundo mbinu kufikia mwaka 2030 ili kuboresha uzalishaji kwa kupunguza urasimu na kuunganisha uwekezaji binafsi na miradi ya mitaji.

Kituo cha kuratibu shughuli za G20 kwa miundo mbinu kwa kuzishirikisha pamoja serikali, sekta binafsi,mabenki ya maendeleo ya kimataifa na mashirika mengine ya kimataifa kitakuwa na makao yake makuu mjini Sydney.

Maskini pia kufaidika

Nchi tajiri zenye maendeleo makubwa ya viwanda pia zimeunga mkono juhudi za kupambana na ukwepaji kodi unaofanywa na kampuni za kimataifa na wakati huo huo zikisisitiza umuhimu wa usalama wa nishati katika malengo ya kukuza uchumi.

Waziri Mkuu wa Australia Tony Abbott amesema faida za ukuaji huo wa uchumi zitaonekana duniani kote na sio tu katika mataifa wanachama wa kundi la G20.

Waandamanaji wakipinga mkutano wa G20 mjini Brisbane.
Waandamanaji wakipinga mkutano wa G20 mjini Brisbane.Picha: picture-alliance/dpa

Amesema Mpango wa Utekelezaji wa Brisbane na mikakati ya kukuza uchumi na mipango ya ajira ya nchi binafsi imetangazwa hadharani ili watu duniani kote waone kujitolea kwao,wawajibishe na kushuhudia hatua zao za maendeleo.

Mkuu wa Benki ya Dunia Jim Young Kim amesema ukuaji mkubwa wa kiuchumi na ulio shirikishi ni muhimu ili kupunguza umaskini na ukosefu wa usawa.Mkuu wa shirika la misaada la Uingereza Oxfam Winnie Byanyima akiunga mkono ujumbe wa Kim amesema kuimarisha ukuaji wa uchumi lazima kuboresha hali ya maisha ya familia za kimaskini na kupunguza ukosefu wa usawa badala tu ya kuwanufaisha matajiri.

Vikwazo zaidi kwa Urusi

Mataifa ya magharibi yametuma ujumbe madhubuti kwa Urusi mwishoni mwa mkutano huo wa kilele wa G20 kwamba lazima ikomeshe kuingilia kati kwake kusikokubalika katika masuala ya Ukraine venginevyo itakabiliwa na vikwazo zaidi.

Rais Barack Obama wa Marekani na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron waliufikisha ujumbe huo wa mataifa ya magharibi wa kudhibiti vitendo vya Urusi katika mkutano huo mjini Brisbane ambapo Rais Vladimir Putin wa Urusi alikabiliwa na shutuma kubwa kutoka kwa viongozi wenzake.

Rais Barack Obama wa Marekani na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani katika mkutano wa G20 mjini Brisbane.
Rais Barack Obama wa Marekani na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani katika mkutano wa G20 mjini Brisbane.Picha: Reuters/Chris Hyde/Pool

Wakati uhusiano kati ya mataifa ya magharibi na Urusi ukiwa mbaya kuwahi kushuhudiwa tokea kumalizika kwa Vita Baridi Obama ameonya kwamba kutengwa kwa Urusi kutaongezeka iwapo nchi hiyo itagoma kubadili mkondo wake.

Urusi kuendelea kutengwa

Kiongozi huyo wa Marekani amewaambia waandishi wa habari baada ya mkutano huo wa kilele kwamba iwapo Putin " ataendelea kufuata njia alioko kwa kukiuka sheria ya kimataifa na kuwapatia silaha nzito waasi wanaotaka kujitenga nchini Ukraine....hapo tena kutengwa kwa Urusi ambako nchi hiyo inakabiliana nako hivi sasa kutaendelea."

Obama amesema serikali ya Marekani inataka kuikaribisha tena Urusi katika jumuiya ya kimataifa lakini kanuni kuu za msingi ziko hatarini.

Rais Barack Obama wa Marekani na Waziri Mkuu wa Canada Stephen Harper mjini Brisbane.
Rais Barack Obama wa Marekani na Waziri Mkuu wa Canada Stephen Harper mjini Brisbane.Picha: Reuters/Reed

Mojawapo ya kanuni hiyo amesema kuwa ni kutozivamia nchi au kuwagharamia vibaraka wake na kuwaunga mkono kwa namna ambavyo huvunja nchi yenye utaratibu wa uchaguzi wa demokrasia.

Cameron amesema mataifa ya magharibi yataendeleza kampeni yake kwa miaka chungu nzima ikibidi kwa sababu mbadala wa hilo ni kuruhusu mzozo wa Ukraine kuendelea kuja "kuwa aina fulani ya mzozo wa kudumu ulioganda katika bara la Ulaya."

Putin aondoka na mapema

Onyo la Obama na Cameron limekuja baada ya Putin kuondoka Brisbane kabla ya hata kutolewa kwa taarifa ya mwisho katika hatua ambayo sio ya kawaida ambayo nayo imekuja kufuatia mfululizo wa majibizano kuhusu Ukraine.

Rais Vladimir Putin wa Urusi akiondoka Brisbane.(16.11.2014)
Rais Vladimir Putin wa Urusi akiondoka Brisbane.(16.11.2014)Picha: Getty Images/R. Maccoll

Bebeduo kubwa limetokea Jumamosi wakati Putin alipomsogelea Waziri Mkuu wa Canada Stephen Harper kupeana naye mkono Harper alimwambia: "Nadhani nigelipokea mkono wako lakini nina jambo moja tu la kusema ....unatakiwa utoke Ukraine."

Putin aliwaambia waandishi wa habari muda mfupi kabla ya kuondoka Brisbane kwamba ilibidi aondoke na mapema kwa sababu alikuwa akihitaji masaa manne hadi matano ya kupumzika kabla ya kuanza kazi hapo Jumatatu.

Putin alikuwa kiongozi wa kwanza kuondoka Brisbane wakati viongozi wenzake wa kundi la G20 wakijipatia mlo wa mchana kwa pamoja na kabla ya kutowa taarifa yao ya kukamilisha mkutano wao huo wa kilele.

Mwandishi : Mohamed Dahman /AFP/AP

Mhariri : Amina Abubakar