1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mchungaji Mackenzie na wenziwe warejeshwa rumande

5 Mei 2023

Mchungaji Paul Makenzie na washukiwa wengine 17 wanaotuhumiwa kwa vifo vya zaidi ya waumini 100 wa madhehebu yenye utata nchini Kenya wataendelea kubakia rumande kwa muda siku tano zaidi.

https://p.dw.com/p/4Qxg3
Polizisten eskortieren Ezekiel Ombok Odero im Polizeipräsidium in Mombasa
Picha: Stringer/REUTERS

Akiwa amevalia koti la rangi ya waridi na suruali ndefu ya kahawia, Paul Makenzie, alifikishwa mbele ya hakimu mkuu mwandamizi Yusuf Shikanda siku ya Ijumaa (Mei 5) pamoja na mkewe, na washukiwa wengine 16 katika Mahakama ya Shanzu mjini Mombasa.

Kupitia wakili wao, washukiwa hao walikuwa wamewasilisha ombi la kuachiliwa kwa dhamana, lakini upande wa mashtaka uliiambia mahakama kuwa "kuachiliwa kwa mshukiwa huyo kunaweza kutatiza shughuli za uchunguzi na vile vile ni hatari kwa usalama wake."

Soma zaidi: Wachungaji wawili wanaotuhumiwa na mauaji kufikishwa mahakamani Kenya

Jami Yamani, wakili mkuu mwandamizi upande wa mashtaka, na wakili Yousuf Aboubakar kutoka shirika la kutetea haki za binaadamu la Haki Afrika waliiomba mahakama kuendelea kuwazuia watuhumiwa hao kwa siku 90 kuruhusu kukamilika kwa uchunguzi unaoendelea.

Polizisten eskortieren Ezekiel Ombok Odero im Polizeipräsidium in Mombasa
Polisi wakimsindikiza Ezekiel Ombok Odero anayetuhumiwa kuhusika na vifo vya waumini wa kanisa la Mchungaji Paul Mackenzie pwani ya Kenya.Picha: Stringer/REUTERS

Mahakama ya Shanzu iliamuru watuhumiwa kurejeshwa rumande hadi itakapotowa uamuzi wa ombi hili mnamo tarehe 10 Mei.

Hakimu Mkuu mwandamizi Yusuf Shikanda pia alitoa maelekezo kuwa washukiwa hao wazuiliwe katika vituo vya polisi vilivyoko Malindi.

Katika Kaunti ya Kilifi, shughuli ya upasuaji wa miili iliyofukuliwa katika msiku wa Shakahola ilikamilika siku ya Ijumaa katika hospitali ya kaunti mjini Malindi.

Ruto ateuwa kikosi kazi 

Huku hayo yakijiri, RaisWilliam Ruto alimteua Kasisi Mutavi Musyimi kuwa mwenyekiti wa kikosi kazi cha kukagua mfumo wa kisheria na udhibiti wa kusimamia mashirika ya kidini.

Askofu wa kanisa la Deliverince Church International, Mark Kariuki, Eli Rop, Askofu Mkuu Maurice Muhatia na Judy Thongori ni miongoni mwa wajumbe wa kikosikazi hicho kitakachofanya kazi hiyo kwa miezi sita.: 

Soma zaidi:Kenya yaanza upasuaji wa miili ya waliofukuliwa huko Shakahola

Kikosi kazi hicho kimepewa jukumu la kubainisha mapungufu na kupendekeza mabadiliko ya sheria na utawala kama njia moja ya kuzuia misimamo mikali ya kidini.

Jopo hilo limeundwa baada ya makaburi ya halaiki kugunduliwa katika Msitu wa Shakahola, Kilifi.

Rais Ruto pia alimteua Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jessie Lessit kuwa mkuu wa tume inayochunguza mauaji ya Shakahola.

Imeandikwa na Halima Gongo/DW Mombasa