Mashambulizi ya Syria Raqqa yauwa raia 95
26 Novemba 2014Ukanda wa video uliopatikana na shirika la habari la reuters uliwaonyesha wakaazi wa mji wa Raqqa wakihamisha mifuko iliyokuwa na miili huku kukiwa na uharibifu mkubwa sana wa majengo ya umma yakiwemo makumbusho ya taifa, msikiti wa Al-Hati na eneo la viwanda.
Shirika la uangalizi wa haki za binaadamu la Syria lenye makao yake mjini London Uingereza, limesema idadi isiyopungua 52 ya waliokufa katika mashambulizi ya ndege za Syria walikuwa raia, lakini halikusema iwapo wengine walikuwa wapiganaji wa Jihadi au raia pia.
Mji wa Raqqa ndiyo ulikuwa mji mkuu wa kwanza wa jimbo kuangukia mikononi mwa waasi na baadae ukachukuliwa na IS, ambayo imeutumia kama mji mkuu wa kile inachokiita Khilafa.
Utawala wa Assad wazidisha mashambulizi
Mashambulizi ya serikali ya Syria yameongezeka tangu Marekani na washirika wake walipoanzisha operesheni dhidi ya kundi hilo ndani ya Syria mwezi Septemba, ambapo katika mwezi uliyopita, jeshi la anga la nchi hiyo limeripotiwa kufanya mashambulizi 1,592 nchini Syria kote, na kuuwa raia 396.
Katika taarifa siku ya Jumatatu, Uongozi wa juu wa jeshi la Marekani ulisema vikosi vya muungano vilifanya mashambulizi kadhaa dhidi ya wapiganaji wa IS tangu Ijumaa wiki iliyopita, tisa nchini Syria na 15 nchini Iraq.
Jeshi la Marekani lilisema mashambulizi nchini Syria, karibu na mji wa mpakani wa Kobani na Raqqa yaliharibu ngome tatu za mapigano za kundi hilo, na kuyalenga maeneo kadhaa na moja ya majengo ya makao yao makuu.
Wamarekani washtakiwa kwa kuiunga mkono IS
Mjini Minneapolis, waendesha mashtaka wa Marekani wamewashtaki wanaume wawili kwa kuiunga mkono IS. Ofisi ya mwanasheria wa Marekani mjini humo imedai katika lalamiko la jinai kuwa Abdi Nur mwenye umri wa miaka 20 na Abdullahi Yusuf mweny eumri wa miaka 18 walishiriki katika njama ya kutoa msaada wa vifaa kwa IS, na kwamba Nur alikuwa ametoa msaada huo. Wanaume hao wawili ni raia wa Marekani wenye asili ya Somalia.
Kulingana na faili la mashtaka dhidi ya wawili hao, Abdullahi Yusuf alisimamishwa na maafisa wa FBI katika uwanja wa ndege wakati akielekea mashariki ya kati mwishoni mwa mwezi Mei, na serikali bado inaendelea kumsaka Abdinur alieondoka kwenda mjini Istanbul Uturuki.
Malaysia yataka kuimarisha sheria za usalama
Na kutoka Kuala Lumpur, waziri mkuu wa Malaysia Najib Razak ameliomba bunge la nchi hiyo kuipa serikali mamlaka zaidi ya kisheria kupambana na wapiganaji wa IS na wafasu wao katika taifa hilo lenye idadi kubwa ya waumini wa Kiislamu Kusini-Mashariki mwa Asia.
Waziri mkuu Razak alisema sheria za sasa za usalama zinahitaji kuimarishwa zaidi kuhakikisha kuwa serikali inachukuwa hatua zenye ufanisi. Polisi imebainisha raia 39 wa Malaysia wanaojihusisha na shughuli za IS nchini Syria, na kwamba imewakamata watu wasiopungua 40 waliokuwa wanapanga kwenda kujiunga na mapigano ambayo IS inayaitia ya Jihad.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae, rtre, ap
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman