Marekani yapanua mashambulizi dhidi ya IS
16 Septemba 2014Mashambulizi hayo ya anga yaliyofanywa na jeshi la Marekani alfajiri ya leo yalikuwa na nia ya kuvisaidia vikosi vya serikali ya Irak Kusini magharibi mwa mji mkuu Baghdad.
Yameelezwa kuwa hatua ya awali kabisa katika operesheni iliyopanuliwa dhidi ya wapiganaji wa kijihadi wa kundi la IS, ambayo jeshi la Marekani limesema itakwenda mbali zaidi ya kulinda usalama wa raia wa Marekani na shughuli za kutoa msaada.
Jeshi hilo limesema mashambulizi haya yanavipiga vituo vya IS, huku jeshi la Irak likisonga mbele dhidi ya kundi hilo, kulingana na mkakati uliotangazwa na rais Barack Obama wiki iliyopita.
Mbinyo kutoka kaskazini
Mbali na Baghdad, Marekani na nchi washirika wameendelea kulisaidia jeshi la Irak na wapiganaji wa kikurdi wajulikanao kama Peshmerga, dhidi ya kundi la IS kaskazini mwa nchi.
Kwa kutumia msaada huo, wapiganaji wa Peshmerga wameweza kurejesha udhibiti wa mji wa Zumar na vijiji vilivyo karibu, ambavyo kwa muda sasa vimekuwa chini ya Taifa la Kiislamu, IS. Kamanda wa Peshmerga Zaeem Ali amezungumzia mafanikio hayo.
''Tumeliarifu jeshi la anga la Marekani kuhusu operesheni yetu katika eneo hili, na tukawapa maelekezo na taarifa zote. Wametusaidia na msaada wao ulikuwa na tija, na tumeridhika. Imetusaidia sana kusonga mbele.'' Amesema kamanda Ali.
Kamanda huyo wa kikurdi amesema katika operesheni hiyo wameweza kuikomboa sehemu yenye urefu wa KM 10, ambalo lina vijiji vipatavyo vitano ndani yake, na kuongeza kuwa kwa wakati huu wamejizatiti kuimarisha ulinzi wa eneo lao.
Kipigo kwa Syria iwapo itajikinga
Na wakati rais Barack Obama tayari amekwishaidhinisha mashambulizi dhidi ya IS ndani ya Syria, Marekani imesema ikiwa jeshi la nchi hiyo litathubutu kuzihujumu ndege za Marekani zitakazohusika katika operesheni hiyo, nchi hiyo italipiza kisasi.
Afisa mmoja wa kimarekani ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema jeshi lao linaelewa vyema vilipo vituo vya anga vya serikali ya Syria, na kuonya kuwa iwapo Syria itajaribu kuizuia operesheni ya Marekani itakuwa ikiziweka ndege zake katika hatari kubwa. Msemaji wa Ikulu ya Marekani Josh Earnest pia ametoa kauli yenye mwelekeo kama huo.
Taarifa zaidi kutoka mashariki ya kati zimeeleza kuwa ndege ya Syria imeanguka kaskazini mwa mji wa Raqqa katika eneo lililo chini ya udhibiti wa kundi la IS, baada ya kufanya mashambulizi katika eneo hilo. Aghalabu jeshi la Syria huwa halitoi tamko lolote kuhusu kuangushwa kwa ndege zake.
Nchini Marekani kwenyewe viongozi wa chama cha Republican watajaribu leo kuwashawishi wabunge wa chama hicho kuunga mkono mpango wa rais Obama dhidi ya IS, huku pia wakitilia maanani kikomo cha mamlaka ya rais huyo katika kuidhinisha matumizi ya nguvu.
Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae/afpe/ape
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman