1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakurdi wafanya operesheni mpya dhidi ya Dola la Kiislamu

Josephat Nyiro Charo20 Novemba 2014

Wapiganaji wa Kikurdi na wanajeshi wa serikali ya Iraq wamefanya mashambulizi mapya jana (19.11.2014) katika maeneo yaliyotekwa na wanamgambo wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS nchini humo.

https://p.dw.com/p/1DqBl
Irak Kurdische Peschmerga-Soldaten im Kampf gegen IS
Picha: Reuters/A. Jadallah

Wakisaidiwa na mashambulizi ya kutokea ya angani ya Marekani wapiganaji wa Kikurdi wa Peshmerga wameyashambulia maeneo yaliyodhibitiwa na kundi la Dola la Kiislamu wakati wa msimu wa kiangazi mwaka huu. Harakati hiyo iliyalenga maeneo katika mikoa ya Diyala na Kirkuk. Maeneo hayo yametekwa na kundi hilo wakati wa operesheni iliyofanywa mnamo mwezi Agosti ambapo kundi la Dola la Kiislamu liliidhibiti theluthi moja ya Iraq.

Kama sehemu ya mashambulizi hayo wapiganaji wa Peshmerga wakishirikiana na vikosi vya Iraq waliikomboa miji ya Sadiya na Jalula mkoani Diyala. Katika mkoa wa Kirkuk, Wakurdi wakisaidiwa na muungano unaoongozwa na Marekani dhidi ya Dola la Kiislamu walilenga kulikomboa eneo karibu na mji wa Karbaroot, kiasi kilometa 35 magharibi mwa mji wa Kirkuk.

Mashambulizi hayo mapya yanakuja huku waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan akikamilisha vipengee vya mwisho vya mpango utakaoiwezesha nchi yake kutoa mafunzo kwa waasi kupambana na wapiganaji wa Dola la Kiislamu nchini Syria. Uturuki imekuwa ikitia na kutoa kuwasaidia wakurdi wanaopigana na kundi hilo katika mji uliozingirwa wa Kobane kwa hofu ya kuimarisha azma ya Wakurdi ya kutaka taifa lao huru nchini humo. Erodgan ameikataa miito inayoitaka Uturuki ichukue jukumu kubwa zaidi katika mapambano dhidi ya Dola la Kiislamu.

Erdogan aikosoa Marekani

Akizungumza jana mjini mjini Ankara rais huyo pia ameikosoa Marekani kwa kushindwa kutimiza masharti ya Uturuki kuchukua jukumu kubwa katika muungano unaopambana na kundi hilo nchini Syria. Uturuki imedai itafanya hivyo kama mkakati maalumu utaandaliwa kumuondoa madarakani rais wa Syria Bashar al Assad, pamoja na kuundwa kwa eneo salama katika mpaka wake na Syria, na utoaji mafunzo kwa wanachama wa jeshi huru la Syria kupambana na utawala wa Assad.

Türkischer Präsident Erdogan
Rais wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: picture-alliance/dpa

Erdogan alisema, "Muungano haujachukua hatua tulizotaka na tulizohimiza zichukuliwe. Tunapitia kipindi ambapo tunashuhudia ishara kadhaa na uwezekano fulani, lakini bila hatua hizi kuchukuliwa Uturuki itaendelea kushukilia msimamo wake wa sasa."

Erdogan ameyasema hayo huku makamu wa rais wa Marekani Joe Biden anatarajiwa kuwasili mjini Ankara hapo kesho kutafuta msimamo wa pamoja na Uturuki katika vita dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu.

Ufaransa kutuma ndege za kivita

Wakati haya yakiarifiwa Ufaransa imetangaza kwamba ndege zake zimezishambulia ngome za Dola la Kiislamu karibu na mji wa Kirkuk nchini Iraq kama sehemu ya harakati mpya, ikiongeza kuwa itatuma ndege sita zaidi za kivita nchini Jordan ili kuimarisha mapambano yake dhidi ya kundi hilo la kiislamu. Waziri wa ulinzi wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian, amesema jana licha ya ufanisi wa mashambulizi ya kutokea angani ambayo yameyaharibu maeneo ya ulinzi yanayodhibitiwa na kundi la Dola la Kiislamu, wanajeshi wa Iraq na wapiganaji wa Kikurdi wa Peshmerga wataendelea kukabiliwa na mashambulizi makali.

US Angriffe auf IS Stellungen in Syrien 23.09.2014
Picha: Reuters/Shawn Nickel/U.S. Air Force

Kamandi kuu ya Marekani imesema muungano unaoongozwa na nchi hiyo umefanya mashambulizi 24 ya kutokea angani tangu Jumatatu wiki hii, mengi yakifanywa karibu na mji wa Kirkuk. Nchini Syria muungano huo umefanya mashambulizi sita ya angani dhidi ya kundi hilo na smoja dhidi ya kundi la "Khorasan" lililojitenga na mtandao wa kigaidi wa al Qaeda.

Kundi la Dola la Kiislamu limewatesa kinyama watu wa makundi madogo ya kidini nchini Syria na Iraq na kufanya mauaji ya kiholela yakiwemo mauaji ya hivi karibuni ya mfanyakazi wa misaada raia wa Marekani Peter Kassig aliyeonyeshwa katika mkanda wa vidio akichinjwa. Raia wawili wa Ufaransa wametambuliwa kuwa miongoni mwa wanamgambo katika vidio hiyo. Serikali ya Ufaransa imewatambua kama Maxime Hauchard na Mickael Dos Santos, wote wakiwa na umri wa miaka 22 na ambao inasema walikwenda Syria Agosti mwaka uliopita.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/APE

Mhariri: Sekione Kitojo