1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakurdi wa Iraq kutuma silaha Kobane

Elizabeth Shoo27 Oktoba 2014

Siku 40 zimepita tangu waasi wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu waanze kushambulia mji wa Kobane uliopo Kaskazini mwa Syria. Hata hivyo wakurdi wa Iraq hawatatuma wapiganaji Kobane kuwasaidia wenzao.

https://p.dw.com/p/1DcZp
Kobane, Syria
Picha: Getty Images/K. Cucel

Wapiganaji wa kikurdi ndio kundi muhimu linalopambana na Dola la Kiislamu nchini Iraq na Syria. Wiki iliyopita bunge la eneo huru la Kurdistan Kaskazini mwa Iraq, lilipitisha mpango wa kutuma wapiganaji 155 wa Peshmerga kuwasaidia wakurdi wenzao walioko vitani Syria. Hata hivyo, msemaji wa serikali ya Kurdistan ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba hawatatuma vikosi vya kwenda kupigana na kundi la Dola la Kiislamu ama IS.

Marekani yabomoa magari ya IS

Kundi hilo bado linaushambulia mji wa Kobane uliopo karibu kabisa na mpaka kati ya Syria na Uturuki. Lakini hadi sasa wapiganaji wa Kikurdi wamefanikiwa kuwazuia waasi hao kuuteka mji wao kabisa. Shirika linalotetea haki za binadamu Syria na lenye makao yake makuu London, limeeleza kwamba katika siku 40 zilizopita watu 815 wamepoteza maisha yao kwenye vita inayoendelea Kobane. Zaidi ya nusu ya waliouwawa ni wapigananji wa IS.

Wasyria 200,000 wamevuka mpaka kuingia Uturuki
Wasyria 200,000 wamevuka mpaka kuingia UturukiPicha: DW/J.Hahn

Watu wapatao 200,000 wameukimbia mji huo na kuingia nchi jirani ya Uturuki. Jumapili ndege za kijeshi za Marekani zilifanya mashambulizi matano ya angani katika mji wa Kobane. Kwa mujibu wa jeshi la Marekani magari saba na jengo moja la IS lililengwa kwenye mashambulizi hayo. Katika nchi jirani ya Iraq vikosi vya serikali vinafanya juhudi kuwarudisha nyuma wapiganaji wa IS. Wanajeshi walifanikiwa kuvikomboa vijiji vinne kutoka katika mikono ya waasi hao.

Waandamanaji wapinga wasalafi

Wakati vita dhidi ya Dola la Kiislamu ikiendelea Iraq na Syria, hapa Ujerumani zaidi ya watu 3,000 waliandamana katika mji wa Cologne, kuwapinga Waislamu wa madhehebu ya salafi wenye msimamo mkali. Inaaminiwa kwamba sehemu kubwa ya watu wanaokwenda kujiunga na mapiganao ya IS kutokea Ujerumani ni wa madhehebu ya salafi.

Polisi wakiwazuia waandamanaji wa mrengo wa kulia mjini Cologne
Polisi wakiwazuia waandamanaji wa mrengo wa kulia mjini ColognePicha: Reuters/Wolfgang Rattay

Wengi wa waandamanaji waliokusanyika Jumapili wanatokea kwenye mrengo wa kulia, ikimaanisha kwamba wanaziunga mkono siasa za kuwapinga watu kutoka nchi za nje kuishi hapa Ujerumani. Baada ya waandamanaji hao kuzua vurugu, polisi waliwashambulia kwa marungu, magari ya kurusha maji na kuwapulizia pilipili machoni. Waandamanaji 17 walitiwa mbaroni huku polisi 44 wakijeruhiwa.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/Reuters/dpa/ap

Mhariri: Yusuf Saumu