1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lebanon huenda ikatumbukia kwenye mzozo zaidi

16 Julai 2021

Jumuiya ya kimataifa imeendelea kuelezea masikitiko yake baada ya Waziri Mkuu mteule wa Lebanon Saad Hariri kujiuzulu. Hatua yake huenda ikalitumbukiza taifa hilo kwenye mzozo mbaya zaidi.

https://p.dw.com/p/3wZFT
Libanon | Designierter Premierminister Hariri trifft Präsident Aoun
Picha: Dalati & Nohra/dpa/picture alliance

Jumuiya ya kimataifa imeendelea kuelezea masikitiko yake baada ya Waziri Mkuu mteule wa Lebanon Saad Hariri kujiuzulu jana Alhamisi. Kuanzia Umoja wa Mataifa, Marekani hadi Ulaya, viongozi wameonyesha kushtushwa na hatua hiyo ya Hariri anayoichukua katikati ya mzozo wa kisiasa na kiuchumi unaoendelea kutokota nchini humo. 

Waziri mkuu Saad Hariri amesema jana wakati akijiuzulu kwamba alishindwa kuunda serikali, ikiwa ni miezi tisa baada ya kukubali kuchukua jukumu hilo wakati taifa hilo lilipokuwa likizama katika mzozo mkubwa kabisa wa kisiasa na kiuchumi. Hariri anakuwa waziri mkuu wa pili mteule kushindwa kuunda serikali katika kipindi cha chini ya miezi 12.

Kumekuwepo na kutupiana lawama kati ya Hariri na rais Michel Aoun anayeongoza vuguvugu la Christian Free Patriotic kuhusiana na kucheleweshwa kuundwa kwa serikali.

Jumuiya ya kimataifa bado inataka kuundwe serikali kabla ya kutoa mamilioni ya misaada ya kiutu baada ya mlipuko wa mwaka jana katika bandari, mjini Beirut lakini ikitoa masharti ya kuundwa kwanza serikali itakayoweza kupambana na ufisadi. Lakini mivutano ya kisiasa imerudisha nyuma juhudi hizo na kuporomosha kwa kiasi kikubwa sarafu na kusababisha gharama za mafuta na dawa kupanda mno. Macron, Guterres kuendeleza jitihada za kuisaidia Lebanon

Libanon Beirut | Großbrand am Hafen | Schwarze Rauchwolken
Mlipuko kwenye bandari ya Beirut umechangia kuongeza mzozo nchini Lebanon na kusababisha serikali kujiuzulu. Picha: Reuters/M. Azakir

Hatua ya Hariri ya kujiuzulu inayochukuliwa takriban mwaka mmoja baada ya mlipuko huo uliosababisha pia serikali kujiuzulu inaurejesha nyuma kabisa mchakato wa kisiasa na kuna hatari iliyo wazi kabisa ya kufuatiwa na miezi kadhaa ya vuta nikuvute.

Jumuiya ya kimataifa yaeleza kuskitishwa na hatua ya Hariri.

Umoja wa mataifa kupitia msemaji wake Eri Kaneko umesema umeshtushwa sana na Lebanon kushindwa kufikia makubaliano ya kuunda serikali mpya na kurejelea mwito wake wa kufikiwa kwa makubaliano ili kuliondoa taifa hilo kwenye mzozo.

"Tunajua kwamba waziri mkuu mteule Saad Hariri amejiuzulu. Tunasikitika kwamba viongozi wa lebanon wameshindwa kukubaliana kuunda serikali mpya. Tunarejea mwito wetu kwa uongozi wa kisiasa kukubaliana bila ya masharti kuunda serikali mpya itakayoweza kushughulikia changamoto kadhaa zinazoikabili nchi. Katibu mkuu na mratibu wake maalumu Joanna Wronecka wataendelea kushirikiana na wadau muhimu kuisaidia Lebanon na watu wake." amesema Kaneko.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Anthony Blinken amesema hatua hiyo ya Hariri imewasikitisha sana. Amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuundwa kwa serikali itakayokuwa na uwezo wa kutekeleza mageuzi muhimu.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian amesema hatua ya Hariri ilikuwa ni uthibitisho kwamba maafisa wa Lebanon hawana uwezo wa kusaka suluhu ya kujiondoa kwenye mzozo uliopo na kuwatuhumu kwa kujiangamiza kijinga wao wenyewe, huku rais Emmanuel Macron akiandaa mkutano wa kimataifa juu ya Lebanon utakaofanyika August 4 wakati ikiadhimisha mwaka mmoja tagu mlipuko wa Beirut 

Rais Aoun sasa atakuwa na jukumu la kuliomba bunge kuchagua waziri mkuu mpya mteule, atakayepewa kazi ya kuunda baraza jipya la mawaziri, ambalo litatakiwa kuidhinishwa na rais na makundi ya kisiasa.

Mashirika: AFPE