Mlipuko mkubwa waua watu 60 mjini Beirut
4 Agosti 2020Maafisa walisema zaidi ya watu 60 wameuawa na wengine zaidi ya 3,000 wamejeruhiwa, huku miili ikiwa imezikwa katika vifusi.
Saa chache baadaye, magari ya kubebea wagonjwa yalikuwa yakiwabeba majeruhi huku helikopta za jeshi zikisaidia kuuzima moto mkubwa uliokuwa ukiendelea kuwaka katika bandari hiyo.
Hospitali za Beirut zimejaa haraka na kukosa mahala pa kuwalaza wagonjwa. Hospitali hizo zimetoa wito zipelekewe damu na majenereta kusaidia kuwa na umeme unaohitajika kwa ajili ya taa.
Chanzo cha mlipuko huo, uliosababisha moto mkubwa, kupindua magari madogo na kuvunja madirisha na milango, hakikujulikana mara moja.
Abbas Ibrahim, Mkuu wa kikosi cha usalama cha Lebanon, alisema huenda moto huo ulisababishwa na nyenzo zenye uwezo mkubwa wa kulipuka zilizokamatwa kwenye meli moja siku chache zilizopita na kuhifadhiwa katika bandari hiyo.
Mlipuko huo ulisikika hadi nchini Cyprus, kilometa zaidi ya 200 upande wa bahari ya Mediterania.
(ape)