1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron aionya Lebanon

6 Agosti 2020

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amekutana na mwenzake wa Lebanon, Michel Aoun pamoja na waziri mkuu Hassan Diab katika makazi ya rais wa Lebanon na kutaka mageuzi ya haraka nchini humo.

https://p.dw.com/p/3gY73
Libanon Macron in Beirut
Picha: Reuters/D. Nohra

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amekutana na mwenzake wa Lebanon, Michel Aoun pamoja na waziri mkuu Hassan Diab katika makazi ya rais wa Lebanon, siku mbili baada ya mlipuko uliosababisha maafa makubwa katika mji mkuu Beirut. Tayari Ufaransa na mataifa mengine yametuma misaada ya dharura na kusaidia timu za uokozi zinazowatafuta watu waliofukiwa na vifusi. 

Sasa taifa hilo ambalo tayari linakabiliwa na mzozo mbaya wa kiuchumi, linakabiliwa na changamoto ya kuujenga upya mji huo mkuu. Hata hivyo bado haiko wazi ni kiasi gani cha msaada utakaotolewa na jamii za kimataifa nchini humo.

Libanon Macron in Beirut
Macron amezungumza na viongozi waandamizi wa Lebanon, ikiwa ni pamoja na rais Aoun kuhusu mustakabali wa taifa hilo.Picha: Reuters/D. Nohra

Macron, aliyetembelea bandari iliyoharibiwa na mlipuko huo na kukutana na maafisa wa ngazi za juu, amesema ziara hiyo ilikuwa ni fursa ya kuwa na majadiliano ya uwazi lakini magumu na viongozi wa kisiasa na wa kitaasisi wa Lebanon. 

Amesema, Ufaransa itashughulika na kuratibu misaada, lakini akionya kwamba iwapo hakutafanyika mageuzi, Lebanon itaendelea kuzama. Alisema "Tutaleta chakula na vifaa ili kuyajenga upya makazi, lakini pia kinachotakiwa hapa ni mabadiliko makubwa ya kisiasa."

Macron aliongeza kuwa "Mlipuko huu unapaswa kuwa mwanzo wa enzi mpya. Hiki ndio kitu cha pekee kinachoweza kuleta mwanzo wa enzi mpya"

Baadae, rais Macron alitembelea makazi yaliyoharibiwa vibaya kabisa na mlipuko huo, na kupokelewa na kundi la raia walioonyesha ghadhabu dhidi ya serikali yao wakipiga kelele wakisema "uhuru" na "watu wanataka kuiondoa serikali, itikadi iliyotumika wakati wa maandamano makubwa ya mwaka jana.

Hata hivyo Macron alisema hakwenda pale kwa lengo la kuirekebisha serikali, na kuapa kwamba msaada ya Ufaransa hautaangukia mikononi mwa wala rushwa.

Libanon, Beirut: Emmanuel Macron
Macron akizungumza na mmoja ya raia wa Lebanon alipotembelea eneo la GemayzehPicha: picture-alliance/dpa/AP/B. Hussein

Gavana wa Beirut Marwan Abboud amekiambia kituo cha televisheni kinachomilikiwa na Saudi Arabia cha Al-Hadath hapo jana kwamba hasara iliyosababishwa na mlipuko huo inakadiriwa kuwa kati ya dola bilioni 10 hadi 15 na karibu watu 300,000 hawana makazi.

Mbali na Ufaransa, Lebanon imekataa msaada kutoka Israel, kutokana na kutokuwepo kwa mahusiano ya kidiplomasia baina ya mataifa hayo ambayo yako katika hali ya kivita, kufuatia kuongezeka kwa wasiwasi kati ya Israel na vuguvugu la Hezbollah la Kishia linaloungwa mkono na Iran katika eneo la mpakani.

Msemaji wa serikali Cyprus Kyriakos Koushos ameliambia shirika la habari la DPA kwamba serikali ya Israel imesema tayari ilipeleka wahudumu wa afya nchini Cyprus ili kuwasaidia watu ambao huenda wangepelekwa kwenye kisiwa hicho kilichopo kilomita 40 kutoka Lebanon.

Hata hivyo, wizara ya mambo ya kigeni ya Israel imekataa kuzungumzia taarifa hiyo.

Mashirika: RTRE/APE/DPAE