Kwanini ulimwengu umewaangusha wanawake kwa kiasi kikubwa?
7 Aprili 2021Athari za janga la corona zinaonekana kupitia kuugua,kifo na kuleta hali ya kukata tamaa kwa watu wengi. Wanawake ni watu wanaoipitia hali hii kila siku kwasababu ndio haswa wanaoubeba mzigo katika janga hili.
Wanawake wameathirika zaidi katika suala la ukosefu wa ajira, wanakabiliwa na ugumu mkubwa wa kupata huduma za afya na mara nyingi ama wanapata kidogo au hawapati kabisa msaada wa kiuchumi au kijamii.
Janga hili limeongeza kwa kiwango kikubwa ukosefu wa usawa wa kijinsia na hiyo ndio mojawapo ya taswira iliyoonekana katika ripoti ya mwaka ya Amnesty Internatinala ya kurasa 408.
Ripoti hii inapaswa kuwafikia moja kwa moja wanasiasa kote ulimwenguni kwasababu hali ya wanawake ni mbaya. Wanahitaji kuungwa mkono na kusaidiwa kwa dhati kabisa lakini katika nchi nyingi hali inayowakabili wanawake hao haishughulikiwi.
Mfano ni nchini India ambako wanawake waliathirika kwa kiasi kikubwa sana kwa kupoteza ajira zao katika kipindi cha wimbi la mwanzo la janga la Corona. Mwezi Machi na Aprili pekee wanawake milioni 15 ghafla walijipata bila kazi na hali iko vivyo hivyo katika mataifa ya Amerika Kusini.
Katika janga hili la corona idadi ya wanawake kukosa kazi imepanda na kufikia asilimia 44. Pia imesahaulika kwamba asilimia 70 ya manesi duniani ni wanawake, na wapo katika hatari kubwa ya kuambukizwa virusi vya corona.
Kwahiyo kunahitajika mikakati dhabiti ya kuwalinda hasa wakati huu. Kingine kinachohitajika ni uongozi. Kuna umuhimu wa kuwa na siasa za kijasiri zinazotambua hali za wanawake, zisizowabagua na kuwatambua wanawake wenyewe.
soma zaidi: Kampeni ya siku 16 kupinga ukatili dhidi ya wanawake Burundi
Lakini kwa sasa hilo halipo, hakuna kipaumbele kinachotolewa katika maeneo ambayo hali ni mbaya. Kwa mfano Unyanyasaji dhidi ya wanawake umeongezeka duniani kutokana na kwamba vituo vya dharura na maeneo mengine yamefungwa kwa zaidi ya mwaka sasa.
Hii inamaanisha kwa mwanamke yoyote aliyefungiwa nyumbani kwaajili ya mashati ya kutotoka nje ili kudhibiti maambukizi ya corona hawezi kuukwepa mkono wa unyanyasaji.
Mexico pekee ilisajili mauaji ya wanawake 969. Hali ni mbaya pia barani ulaya, wanawake 19 waliripotiwa kuuwawa na wapenzi wao. Brazil, na Paraguay hali hairidhishi sana, kwa ufupi ni maeneo mengi duniani ambako wanawake hawako salama.
Ni lazima hatua ichukuliwe, ni lazime wanawake wasaidiwe maana wana haki ya kuishi kwa heshima na bila uwoga mahali popote pale.
Mwandishi: Manuela Kasper-Claridge/Amina Abubakar