1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kisa cha kwanza cha Corona charipotiwa Lagos,Nigeria

28 Februari 2020

Maafisa wa afya nchini Nigeria wameripoti kisa cha kwanza cha virusi vya Corona mjini Lagos. Taifa hilo limekuwa la kwanza katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara kukumbwa na virusi hivyo.

https://p.dw.com/p/3YaOP
Afrika Sambia Coronavirus Vorkehrungen
Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Mwiche

Kamishna wa Afya mjini Lagos, mji mkubwa barani Afrika ulio na idadi jumla ya watu milioni 20 amesema raia mmoja wa Italia aliyeingia Nigeria siku ya Jumanne kutoka Milan, akiwa katika safari zake za kibiashara aliugua siku ya pili yake.

Kamishna Akin Abayomi amesema mtu huyo aliwekwa karantini na kuanza mara moja kufanyiwa vipimo katika hospitali moja mjini humo, huku akisema maafisa wake wanajaribu kuchunguza  ni akina nani mwanamume huyo aliyeingiliana nao tangu alipoingia  mjini Lagos.

Mapema mwezi huu maafisa mjini humo walitoa ushauri kwa watu wote wanaoingia huko kutoka China, kujiweka karantini kwa muda wa siku 14 ambao ndio muda unaoweza kugundua iwapo mtu ameambukizwa au la.

Huku hayo yakiarifiwa Iran imeripoti kufuta sala zote za Ijumaa mjini Tehran na kote katika Jamhuri hiyo ya kiislamu kufuatia mripuko wa virusi hivyo vinavyojulikana kama COVID-19 Tangazo hilo lilitolewa hapo jana baada ya idadi ya walioambukizwa virusi hivyo kupanda kutoka watu 100 hadi watu 254 huku watu 26 wakiwa wameshafariki dunia.

Iran ndio taifa lililo na idadi kubwa ya watu waliofariki nje ya China kulikoanzia mripuko huo wa virusi vya Corona vinavyoendelea kuzua wasiwasi wa kuenea zaidi katika eneo la Mashariki ya Kati.

Saudi Arabia yachukua mikakati ya kujikinga na Corona

Coronavirus SARS-CoV-2 im Elektronenmikroskop
Picha: picture-alliance/AP/NIAID-RML

Saudi Arabia kwa upande wake imechukua hatua za kujikinga na virusi hivyo kwa kupiga marufuku mahujaji wa kigeni kuingia nchini humo kuzuru maeneo matakatifu kwa waumini wa dini ya kiislamu hatua iliyovuruga pia mipango ya mamilioni ya mahujaji kuelekea katika ibada ya Hijaa inayofanywa kila mwaka nchini humo.  Bado hapajakuwa na kisa chochote cha virusi hivyo nchini Saudi Arabia.

Kwengineko Rais wa Mongolia Battulga Khaltmaa pamoja na maafisa wengine wa serikali wamejiweka karantini kwa siku 14 baada ya kurejea nyumbani kutoka ziara yao nchini China hii ikiwa ni kulingana na shirika la habari la kitaifa nchini humo.

Battulga ndio rais wa kwanza kuizuru China tangu taifa hilo lilipoanza kuchukua mikakati maalum kujaribu kudhibiti virusi hivyo tangu vilipoanza mwezi wa Januari. Rais Battulga Khaltmaa aliwasili mjini Beijing pamoja na waziri wake wa mambo ya kigeni Tsogtbaatar Damdin na maafisa wengine wa serikali hapo jana na kukutana na rais Xi Jinping na Waziri Mkuu Li Keqiang.

Watu zaidi ya 83,000 duniani wameambukizwa virusi vya Corona huku China bara mahala kulikoanzia mripuko wa virusi hivyo ikiripoti vifo vya watu 2,788 huku watu zaidi ya 78,824 wakiambukizwa hasa katika mji wa Hubei.

Chanzo: /AP/Reuters