Ujerumani yachukua hatua kuzuwia kusambaa virusi vya Corona
27 Februari 2020Serikali ya Italia nayo ikihangaika kuzuwia mdororo wa uchumi, inajitahidi kupuuzia hali mbaya ya maambukizi ya virusi vya Corona nchini humo, ikiwa ni nchi pekee ya Ulaya ambayo imeathirika zaidi.
Watu mia kadhaa wamewekwa chini ya karantini majumbani mwao katika jimbo lenye wakaazi wengi la upande wa magharibi mwa Ujerumani la North Rhine Westfalia baada ya mwalimu wa shule ya chekechea , aliyeshiriki katika sherehe za kitamaduni za Kanivali , kuthibitishwa kuwa ameambukizwa na virusi vya Corona.
Wale waliwekwa chini ya karantini wamebakia majumbani mwao kwa siku 14 wakati marafiki na ndugu wakiwapelekea mahitaji ya chakula na kadhalika, wakiviweka vitu hivyo nje mlangoni na kuepuka kugusana nao. takriban watu 10 wapya wamethibitishwa kuwa na virusi hivyo vya Corona nchini Ujerumani, na msako wa watu wengine walioathirika umeendelea leo Alhamis.
Mkuu wa kitengo cha nje katika halmashauri ya viwanda na biashara nchini Ujerumani DIHK, Volker Treier, ametabiri kwamba uchumi wa Ujerumani utaathirika sana katika mwaka huu 2020.
Idadi ya vifo yapanda
Nchini Italia, nchi ambayo imeathirika zaidi katika mataifa ya Ulaya, mbali ya mawaziri kutoa ujumbe wa uhakikisho , maafisa wanasema idadi ya vifo imepanda kwa watu wawili na kufikia watu 14 usiku wa jana, wakati idadi ya watu ambao wamethibitika kuwa wameambukizwa ugonjwa huo imepanda kwa zaidi ya watu 100 na kufikia watu 528.
"Janga la kutoa taarifa za upotoshaji litaleta madhara makubwa zaidi nchini Italia kuliko hatari ya janga la virusi vyenyewe," waziri wa mambo ya kigeni Luigi Di Maio alisema katika mkutano na waandishi habari. Ni moja tu asilimia ya nchi ambayo inahusika na ugonjwa huo, ameongeza Di Maio.
Mashirika ya habari ambayo si ya serikali nchini Iran yameripoti kuwa swala ya Ijumaa imefutwa mjini Tehran na kwingineko katika jamhuri hiyo ya Kiislamu kuhusiana na kuzuka kwa virusi hivyo.
Taarifa hizo zimejitokeza leo wakati Iran imekuwa na ongezeko la watu walioambukizwa virusi hivyo kwa zaidi ya watu 100 na kufikisha watu 254.
Wakati huo huo nchi hiyo imechukua hatua ya kupiga marufuku raia wa China kuingia nchini humo, shirika la habari la Iran IRNA limeripoti leo, kutokana na kusambaa kwa virusi vya Corona katika taifa hilo.
Saudi Arabia imesitisha safari kwenda katika maeneo takatifu nchini humo, kwa watu kutoka mataifa yaliyoathirika zaidi na virusi vya Corona, na Korea kusini imeimarisha adhabu kwa wale watakaokiuka amri ya karantini na maafisa wa viwanja vya ndege katika mataifa ya Amerika kusini wanaangalia ishara kumtambua abiria mgonjwa, wakati virusi hivyo vikiendelea kusambaa kote duniani.