Msitu wa Shakahola kugeuzwa kituo cha kumbukumbu ya kitaifa
9 Juni 2023Kugunduliwa kwa makaburi ya halaiki katika msitu wa Shakahola, eneo la hekta 325 (ekari 800) ambalo liko bara kutoka mji wa Malindi katika Bahari ya Hindi, kumewashangaza Wakenya.
Kiongozi wa madhehebu ya kidini Paul Nthenge Mackenzie anakabiliwa na mashtaka mbalimbali katika kisa hicho cha kutisha, anayedaiwa kuwaendesha wafuasi wake hadi kifo kwa kuhubiri kwamba njaa ndiyo njia pekee ya kuelekea kwa Mungu.
Soma pia: Kenya yaanza upasuaji wa miili ya waliofukuliwa huko Shakahola
Msitu "ambako uhalifu mkubwa umefanyika hautasalia kama ulivyokuwa," waziri wa mambo ya ndani Kithure Kindiki alisema Jumanne. "Serikali itaugeuza kuwa kumbukumbu ya kitaifa, mahali pa ukumbusho ili Wakenya na ulimwengu wasisahau yaliyojiri hapa,” alisema kwenye taarifa.
Wachunguzi walianza awamu ya tatu ya uchimbaji wa makaburi siku ya Jumanne, na kupata miili tisa zaidi iliyofikisha idadi ya waliofariki kufikia 264.
Kindiki alisema shughuli za kundi hilo zilienea zaidi ya msitu wa Shakahola na kwamba uchunguzi "wa kina, wa kitabibu na kisayansi" umeenea hadi kwenye ranchi katika eneo hilo lenye zaidi ya hekta 14,980 (ekari 37,000).
"Pindi zoezi linaloendelea kukamilika, usharika wa waumini wa dini zote na uongozi wa kitaifa utakutana kwa ajili ya ibada ya ukumbusho,” alisema Kindiki.
Uchunguzi: Baadhi ya wahanga waliuawa kwa maksudi
Wakati njaa inaonekana kuwa sababu kuu ya vifo, baadhi ya wahanga -- ikiwa ni pamoja na watoto - walinyongwa, kupigwa au kukoseshwa pumzi, kulingana na uchunguzi wa maiti uliyofanywa na serikali.
Mackenzie -- dereva wa teksi-aliyegeuka-mhubiri -- bado hajahitajika kukiri au kukana makosa, huku upande wa mashtaka ukitaka aendelee kuwekwa kizuizini akisubiri uchunguzi zaidi.
Mwanzilishi wa Kanisa la Good News International mwenye umri wa miaka 50 alijisalimisha mnamo Aprili 14 baada ya polisi kuchukua tahadhari kuingia msitu wa Shakahola. Polisi inasema watu wasiopungua 45 wamekamatwa.
Takriban watu 95 wameokolewa kutoka msituni huku idadi ya walioripotiwa kutoweka ikiwa 613, kulingana na rekodi za polisi. Maswali yameibuka kuhusu jinsi Mackenzie, baba wa watoto saba, alivyoweza kukwepa wasimamizi wa sheria licha ya historia ya itikadi kali na kesi za kisheria za hapo awali.
Sakata hilo la kutisha lilipelekea Rais William Ruto kuunda tume ya uchunguzi kuhusu vifo hivyo na jopo kazi kukagua kanuni zinazosimamia mashirika ya kidini.
Juhudi za kudhibiti dini katika nchi hiyo yenye Wakristo wengi zimepingwa vikali katika siku za nyuma kama majaribio ya kudhoofisha uhakikisho wa kikatiba wa mgawanyiko wa kanisa na serikali.
Chanzo: afpe