Jeshi la Iraq lapata mafanikio Ramadi
28 Desemba 2015Katika taarifa yake iliyotangazwa kwa njia ya televisheni, msemaji wa jeshi la Iraq Jenerali Yahya Rasool alitangaza awali kuwa mji wa Ramadi umekombolewa kutoka katika "kucha za chuki" za kundi la Dola la Kiislamu IS na kwamba mji huo ulikuwa umekombolewa kikamilifu.
"Mji wa Ramadi umekombolewa. Vikosi vya ulinzi vya Iraq vimepandisha bendera ya Iraq kwenye majengo ya serikali. Bendera ya iraq sasa inapepea juu ya jengo la serikali," alisema Jenerali Yahya Rasool.
Lakini Jenerali Ismail al-Mahlawi, mkuu wa operesheni za kijeshi mkoani Anbar, aliingilia haraka na kutoa ufafanuzi kwamba vikosi vya serikali viliyatwaa tu majengo ya kimkakakati ya utawala, na kwamba sehemu za mji huo zimeendelea kuwa chini ya udhibiti wa IS.
"IS wamejiondoa kwenye asilimia 70 ya mji, lakini bado wanadhibiti maeneo mengine na vikosi vya serikali havina udhibiti wa wilaya nyingi ambako wapiganaji wa IS wamekimbilia," alisema al-Mahlawi katika mahojiano na shirika la habari la Marekani - Associated Press, na kuongeza kuwa hawawezi kusema kuwa Ramadi imekombolewa kikamilifu.
Mji wenye historia ya upinzani
Ramadi, ambao ndiyo mji mkuu wa mkoa wa Anbar ulikuwa mmoja ya miji ya Iraq iliyokuwa chini ya udhibiti kamili wa kundi la Dola la Kiislamu au Daesh kama linavyojulikana kwa Kiarabu.
Mji huo pamoja na mingine mkoani Anbar ilishuhudia mapigano makali zaidi kati ya wanajeshi wa Marekani na mtangulizi wa IS - kundi la Al-Qaeda nchini Iraq, katika miaka iliyofuatia uvamizi wa Marekani uliyomuondoa madarakani rais Saddam Hussein mwaka 2003.
Msemaji wa jeshi la Marekani nchini Iraq Kanali Steve Warren, aliiambia AP kuwa ushindi wa Jumatatu ni wa kujivunia kwa Iraq, na kuongeza kuwa kukombolewa kwa majengo ya serikali ni mafanikio muhimu, ambayo yametokana na muda mrefu wa kujituma kwa jeshi la Iraq, vikosi vya kupambana na ugaidi, jeshi la anga, vikosi vya polisi na wapiganaji wa kikabila.
Aliongeza kuwa muungano unaoongozwa na Marekani umetoa msaada kwa serikali ya Iraq kwa kufanya mashambulizi zaidi ya 630, mafunzo kwa wanajeshi, na pia kutoa ushauri maalumu na vifaa vya kuondoa mabomu na mitego.
IS bado inadhibiti maeneo makubwa
Jeshi la Iraq lilianzisha kampeni yake iliyoahidiwa kwa muda mrefu kuukomboa mji wa Ramadi, uliyoko umbali wa kilomita 130 mashariki mwa mji mkuu wa Iraq Baghdad wiki iliyopita.
Lakini operesheni yao ilikabiliwa na vizingiti kadhaa vikiwemo walenga shabaha, mabomu ya mitego na kuharibiwa kwa madaraja yote yanayoelekea mjini Ramadi na wapiganaji wa IS.
Wapiganaji hao wenye itikadi kali za dini bado wanadhibiti maeneo makubwa magharibi na kaskazini mwa Iraq na katika nchi jirani ya Syria. Kundi hilo la IS limetangaza utawala wa khalifa katika maeneo linayoyadhibiti.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape,afpe.
Mhariri: Mohammed Khelef