Jeshi la Iraq lakaribia kukomboa Ramadi
25 Desemba 2015Wanajeshi wa Iraq wamepambana na wapiganaji wa mwisho wa kundi la Dola la Kiislamu waliojificha katika mji wa Ramadi, huku wakipunguza kasi yao kutokana na mashambulizi makali, mitego ya mabomu na hofu ya raia waliokwama mjini humo.
Mapigano yalipamba moto karibu na makao makuu ya serikali mjini Ramadi, eneo muhimu ambalo ikiwa litakombolewa upya na vikosi vya serikali itakuwa hatua nyingine kubwa katika kuuokomboa mji huo ulioanguka mikononi mwa Dola la Kiislamu mwezi Mei.
Mji wa Ramadi umeharibiwa kwa kiasi kikubwa katika miezi kadhaa ya mapigano, na kamanda wa jeshi la Iraq anasema baadhi ya nyumba zilizotegwa mabomu ilibidi ziteguliwe kwa kutumia kifaa cha rimoti ili kuepusha hasara ya vifo au majeruhi ya raia.
Luteni kanali wa jeshi la Iraq amesema wanajeshi wa Iraq wamefika katika kitongoji cha Hoz, karibu mita 500 kutoka kwa ofisi za serikali.
Mkuu wa baraza la mkoa wa Anbar Sabah Karhout anasema idadi kubwa ya mabomu yaliyotegwa na wapiganaji wa IS katika mji huo na uwezekano wa raia waliokwama ambao wanatumiwa kama ngao ya binadaamu ndizo sababu za kuchelewesha juhudi za majeshi ya serikali kuingia mjini humo kwa kasi.
Msemaji wa jeshi la muungano unaoongozwa na Marekani, Kanali Steve Warren amesema IS imewaweka wapiganaji karibu 100 katika barabara inaoyelekea katika jengo la ofisi za serikali.
Taarifa zilizotolewa na IS, zilizungumzia idadi kubwa ya majeruhi na vifo miongoni mwa wanajeshi wa serikali ikiwa ni pamoja na katika shambulizi ililosema ilifanya na walipuaji watano wa kujitoa mhanga mapema jana magharibi mwa Ramadi.
Jeshi la Iraq limetoa upande mwingine wa shambulizi hilo, likisema washambuliaji waliuawa na risasi za polisi au mabomu yao waliyoyalipua kabla ya kufika katika eneo walilolenga.
Kwa mujibu wa Warren, ndege za jeshi la muungano ziliangusha mabomu 50 katika ngome za IS Jumatano pekee. Operesheni ya kuukomboa tena mji wa Ramadi ilianza miezi kadhaa iliyopita huku wanajeshi wa Iraq wakifunga barabara za kupitishia vifaa na bidhaa za kutumiwa na IS katika maeneo ya Anbar kabla ya kuanza kuukaribia mji hio taratibu, huku wakiyadhibiti madaraja muhimu, barabara na maeneo mengine.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohamed Khelef