Spika wa bunge la Iraqi avipongeza vikosi vya serikali
28 Desemba 2015Hatua ya kuudhibiti mji wa Ramadi ambao ni mji mkuu wa jimbo la Anbar lenye waisilamu wengi wa madhehebu ya Sunni inaonekana kuwa pigo kubwa kwa kundi la Dola la Kiisilamu katika kipindi cha mwaka huu wa 2015.
Wanamgambo hao walifanikiwa kuuteka mji huo mwezi Mei mwaka jana baada ya kuvizidi nguvu vikosi vya serikali, hatua iliyopelekea Marekani kuzidisha mikakati yake katika mapambano dhidi ya wanamgambo wa kundi hilo.
Ingawa kuna maeneo ambayo bado wanamgambo hao wanaonekana kuwepo, majeshi ya Iraq yanasema hayahofii kupata upinzani wowote na maafisa wa vikosi vya nchi hiyo tayari walikuwa wakijipongeza kwa kuukomboa mji huo .
Watu waliokuwa wakipeperusha bendera za taifa la Iraqi wameingia katika miji kadhaa ya nchi, ukiwemo mji mkuu Baghdad na mji wa Karbala ambao ni mtakatifu kwa waislamu wa madhehebu ya Shia, kushangilia kukombolewa kwa mji wa Ramadi.
Spika wa Bunge la Iraq Salim al-Juburi alitoa taarifa kupitia vyombo vya habari, akiwapongeza wanajeshi aliowaita 'mashujaa'' kwa kuukomboa mji kutoka katika mikono ya IS.
Muungano wa majeshi yanayoongozwa na Marekani ambao pia ulihusika katika kuyaunga mkono majeshi ya Iraq mjini Ramadi nao pia uliwapongeza kwa mafanikio ya operesheni hiyo ambayo walianza mara tu baada ya kuupoteza mji huo na kuuacha katika himaya ya kundi la IS mwezi Mei.
Majeshi ya Iraq yakiungwa mkono na mashambulizi ya anga kutoka kwa majeshi ya muungano yanayoongozwa na Marekani yalikuwa tayari yameingia katika maeneo ya katikati ya mji wa Ramadi Jumanne ya wiki iliyopita katika harakati zake za mwisho za mapambano ya kuukomboa mji huo.
Mapigano yajikita katika majengo ya serikali
Mapigano katika kipindi cha siku mbili zilizopita yalijikita zaidi katika maeneo yenye majengo ya serikali, hii ikiwa kwa mujibu wa vyanzo vya madakitari
wapiganaji 93 wa vikosi vya serikali walifikishwa hospitalini hapo jana wakiwa na majeraha huku miili ya wapiganaji wa vikosi vya serikali waliouawa katika mapigano ikipelekwa katika hospitali ya jeshi iliyoko karibu na uwanja wa ndege.
Hata hivyo licha ya hatua ya vikosi vya Iraq kutangaza kuukomboa mji huo muungano wa majeshi unaongozwa na Marekani katika kampeni dhidi ya kundi hilo la kigaidi umesema hauwezi kuthibitisha taarifa hizo.
Mwandishi : Isaac Gamba/ AFPE/ RTRE
Mhariri : Gakuba Daniel