1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Italia kuwapokea wafungwa 3 wa Guantanamo

16 Juni 2009

Italia imeridhia kuwachukua wafungwa watatu waliokuwa wakizuiliwa katika jela la Guantanamo iliyoko Cuba.Kauli hizo zimetolewa baada ya Rais Barack Obama wa Marekani kukutana mjini Washington na Waziri Mkuu wa Italia

https://p.dw.com/p/IAYN
Rais Obama akizungumza na Waziri mkuu wa Italia Silvio BerlusconiPicha: AP

Rais Obama aliahidi kulifunga jela hilo ifikapo mwishoni mwa mwaka huu na amekuwa katika harakati za kuzishawishi serikali nyengine za bara la Ulaya kuridhia kuwahifadhi baadhi ya wafungwa wanaoaminika kuwa hawana hatari yoyote tena.Jela la Guantanamo lilifunguliwa punde baada ya mashambulio ya mabomu yaliyotokea Washington na Newyork mwezi Septemba mwaka 2001.


Tangazo hilo la Italia limetolewa baada ya Marekani na Umoja wa Ulaya kuafikiana hapo jana kuwa na mpango maalum utakaoyawezesha mataifa wanachama wa umoja huo kuwapokea baadhi ya wafungwa wa Guantanamo.Kulingana na Rais Obama kauli za serikali ya Italia zinaonyesha kuwa nchi hiyo inaunga mkono harakati zake za kulifunga jela la Guantanamo.Rais Obama alifafanua kuwa hatua hiyo itawapa fursa ya kutunga sheria mwafaka za kimataifa zitakazopambana na ugaidi jambo litakalowanufaisha wahusika wote alisema ''Itakapohitajika chini ya misingi ya sheria na usalama wa kitaifa tutajaribu kuwahamishia baadhi ya wafungwa katika magereza maalum yanayotumiwa kuwazuia wahalifu hatari kote nchini.Tunapochukua uamuzi huu kumbukeni ya kwamba hakuna mtu hata mmoja aliyefanikiwa kutoroka kwenye magereza ya nchi hii yaliyo na ulinzi mkali.''


Uigurische Häftlinge auf Guantanamo
Mlinzi nje ya sehemu wanakozuiliwa wafungwa wa kabila la Uighur wa ChinaPicha: AP

Wiki iliyopita serikali ya Marekani iliwaregesha nyumbani kwao wafungwa watatu wa Saudia,mmoja wa Iraq na mmoja wa Chad.Wengine wanne wa kabila la Uighur liliko China ambao wamezuiliwa kwa kipindi cha miaka minne katika jela hilo walihamishiwa kisiwa cha Bermuda kilicho karibu na Bahari ya Atlantiki.Kwa sasa serikali ya Marekani inaendelea na mazungumzo yaliyo na azma ya kuwasafirisha wafungwa wengine 13 wa Kichina ambao ni waislamu hadi kisiwa cha Palau kilichoko karibu na bahari ya Pasifiki.Marekani imekataa katakata kuwasafirisha wafungwa hao hadi nchini mwao kwa kuchelea kuwa watateswa pindi wafikapo.

Gefangenenlager Guantanamo auf Kuba Flash-Galerie
Jela la GuantanamoPicha: AP

Taarifa nyengine zinaeleza kuwa Marekani huenda ikafikia makubaliano mengine yatakayoiwezesha kuwasafirisha wafungwa 100 wa Kiyemeni waliosalia hadi Saudi Arabia.Wayemeni ndiwo wengi zaidi kati ya wafungwa wote wanaozuiliwa katika jela la Guantanamo.Marekani inaipinga hatua ya kuwarejesha kwao kwani inaamini kuwa hali ya usalama nchini Yemen si nzuri.Kwa sasa wamesalia wafungwa 226 wanaozuiliwa kwenye jela la Guantanamo linalozua mitazamo tofauti.

Punde baada ya kuingia madarakani tarehe 20 mwezi Januari mwaka huu Rais Obama alitangaza kuwa jela la Guantanamo litafungwa katika kipindi cha mwaka mmoja.Hatua hiyo ina azma ya kuibadili taswira ya Marekani katika mataifa ya kigeni.Jela la Guantanamo lilifunguliwa mara baada ya mashambulio ya mabomu yaliyotokea mwezi Septemba mwaka 2001 wakati wa utawala wa George W Bush.Wafungwa hao wamekuwa wakizuiliwa katika jela hilo bila ya kufunguliwa mashtaka rasmi.Makundi ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakililalamikia hilo kwasababu wafungwa hao walikuwa wanateswa.

Rais Obama kwa upande wake anajaribu kuwashawishi viongozi wa mataifa wandani wake kuridhia kuwachukua baadhi ya wafungwa hao.


Bunge la Marekani kwa upande wake linapinga vikali hatua ya kuwahamishia wafungwa hao kwenye magereza nchini humo.Rais Obama amesisitiza kuwa baadhi ya wafungwa ambao hawana kitisho watazuiliwa kwenye magereza ya nchi hiyo na alifafanua kuwa''Hatutamuachia mfungwa yeyote ikiwa hilo litahatarisha usalama wa kitaifa au wafungwa wowote hapa Marekani ikiwa watahatarisha usalama wa raia wa Marekani.''


Zaidi ya wafungwa 540 tayari wameshahamishwa kutoka jela hilo na kupelekwa kwenye mataifa yapatayo 30 tangu mwaka 2002.Hata hivyo kiasi cha wafungwa 230 bado wanazuiliwa Guantanamo kwa sasa.

Mbali ya Italia mataifa 6 mengine barani Ulaya yamesema kuwa huenda yatawapokea baadhi ya wafungwa hao.Mataifa hayo ni Ubelgiji,Uingereza,Ufaransa,Ireland,Ureno na Uhispania.


Mwandishi:Thelma Mwadzaya AFPE /RTRE

Mhariri:M.Abdul-Rahman