1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya na wafungwa wa Guantanamo

4 Juni 2009

Sharti la kuwapokea ni kupashana habari juu yao.

https://p.dw.com/p/I3YA
Wafungwa wa GuantanamoPicha: dpa

Mawaziri wa mambo ya ndani wa nchi 27 za Umoja wa Ulaya,wameafikiana leo wakati wa mkutano wao mjini Luxembourg kuwa , nchi zilizojitolea kuwapokea wafungwa watakaotolewa gereza la Guantanamo,kisiwani Kuba,zitapashana habari kamili zinazowahusu wafungwa hao kabla hazikupitisha uamuzi wa mwisho kuwapokea .

Kamishna wa mambo ya sheria wa Umoja wa ulaya ,Jacques Barrot alisistiza kuwa mfungwa yeyote atakaetolewa kutoka gereza la Guantanamo atakuwa ni mfungwa alieonekana hana hatia.

Nchi zanachama wa Umoja wa Ulaya na zile za eneo la makubaliano ya Shengen lazima ziamue cha kufanya pale wafungwa hao watakaoachiwa na wakipokewa na nchi zanachama wa Umoja wa Ulaya.Nchi zilizofunga mkataba wa Schengen,lazima zipewe fursa ya kuibadilishana taarifa na mafaili yanayowahusu wafungwa hao.Hii alidai hasa waziri wa ndani wa Jamhuri ya Czech,Martin Pecina, ambae nchi yake ya ni mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Ulaya.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Bw.Wolfgang Schauble aliuambia mkutano wa Luxembourg kuwa Ujerumani, itawafungulia tu mlango wale wafungwa wenye mafungamano na Ujerumani na ambao wameonekana si kitisho kwa usalama wake na wenye sababu za kuaminika kwanini hawataki kubakia Marekani.

Bw.Schauble akasema,

"Ikiwa serfikali zote za mikoa ya Marekani hazithubutu kuwapokea wafungwa hao,inatupasa kuwaeleza wakaazi wa ulaya , kwanini kuna kanuni tofauti kwa Marekani na Ulaya."

Waziri wa ndani wa Jamhuri ya Czech na mwenzake wa Austria,Maria Fekter wamearifu kuwa nchi zao haziko tayari kuwapokea wafungwa wowote watakaoachiwa Marekani.

Eneo la nchi zilizofunga mkataba wa SCHENGEN jumla yake ni 22 za Umoja wa Ulaya pamoja na Iceland,Norway na Uswisi zisizo-wanachama na unawaruhusu wakaazi wake kutembelea mojawapo ya nchi hizo nyengine bila ya kiziuzi mpakani.

Kwa muujibu wa makubaliano ya Schengen ,nchi zilizofunga mapatano hayo zinaruhusiwa kuwasusia wakaazi wa nchi zanachama ikiwa wataonekana ni kitisho kwa usalama.

Hatahivyo, waziri wa ndani wa Ujerumani ameikataa fikra kuwa Umoja wa Ulaya uweke vikwazo vya usafiri vya aina hiyo kwa wafungwa wa zamani wa Gereza la Gua ntanamo akidai kwa sasa hakuna haja kama hiyo.

Mapatano yaliofikiwa Luxembourg na mawaziri hao 27 wa nchi zanachama wa Umoja wa Ulaya, yanadai jukumu kubwa la kulifunga Gereza la Guantanamo na kuwatafutia wafungwa wake mahala pa kuhamia , limo mikononi mwa serikali ya Marekani.

Pia zimeamua ni jukumu la kila nchi mwanachama kujiamulia iwapo itayari kuwapokea wafungwa hao watakaoachiwa kutoka Guantanamo.Rais Barack Obama wa Marekani ametangaza hadi mwakani kulifunga kabisa gereza la Guantanamo.

Muandishi: Ramadhan Ali/DPAE

Mhariri: M.Abdul-Rahman