Ujerumani yaombwa iwapokee wafungwa wa Guantanamo
4 Mei 2009Marekani imeiomba Ujerumani iwapokee wafungwa wa zamani wa jela ya Guantanamo.Amesema hayo msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya serikali kuu ya Ujerumani mjini Berlin.
Orodha ya majina ya wafungwa husika imeshakabidhiwa serikali na itawasilishwa wizara ya mambo ya ndani ambayo ndio itakayoamua kama wafungwa hao wa zamani wa Guantanamo wapokelewe humu nchini au la.
"Nnaweza kuthibitisha kwamba maombi rasmi ya Marekani yameshatolewa na majina kutajwa.Wizara ya mambo ya ndani itaanza kulijadili suala hilo mapema wiki hii,pengine kuanzia jumatatu"-msemaji huyo amesema.
Kwa mujibu wa toleo la leo la jarida la Der Spiegel maombi ya serikali ya Washington yanawahusu wafungwa kama kumi hivi wa zamani.Hata hivyo msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya Ujerumani hajathibitisha idadi hiyo.
Kwa mujibu wa gazeti la Bild,wafungwa hao ni wa kabila ya Ouighor,watu wa jamii ya wachache nchini China wanaosema wanasumbuliwa nchini mwao.
Nchini Ujerumani jamii hiyo inakutikana katika jimbo la kusini la Bavaria wanakoishi zaidi ya waouighor mia tano-idadi kubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa ulimwenguni.
Waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la Bavaria,Joachim Herrmann amesema
"La muhimu kabla ya yote ni kwa Marekani kuthibitisha hakuna kitisho chochote cha kigaidi kinachoweza kutokana na wafungwa hao.Tunaamini hawajafuingwa bure katika jela ya Guantanamo.Wizara kuu ya mambo ya ndani ikishapatiwa ufafanuzi na thibitisho timamu ndipo sisi huku Bavaria tutakapolishughulikia suala hilo."
Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya serikali kuu ya Ujerumani mjini Berlin amesema uamuzi utapitishwa baada ya kesi moja moja kuchunguzwa na kwa mashauriano pamoja na nchi nyengine za Umoja wa Ulaya na majimbo yote 16 ya shirikisho la jamhuri ya Ujerumani.
Amekumbusha Ujerumani hailazimiki kuwapokea wafungwa hao.
Serikali kuu ya muungano haina msimamo mmoja kuhusu suala hilo:Waziri wa mambo ya nje Frank-Walter Steinmeier wa kutoka chama cha Social Democratic-SPD,alimwambia rais Barack Obama serikali ya mjini Berlin iko tayari kuwapokea wafungwa hao wa zamani.Lakini waziri wa mambo ya ndani,wa kutoka chama cha kansela Angela Merkel cha Christian Democratic CDU Wolfgang Schäuble anasema anaipinga fikra hiyo.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir
Mhariri Josephat Charo