Iran yafunga waandishi wawili miaka 7 jela
22 Oktoba 2023Wote wawili wamekuwa kizuizini kwa zaidi ya mwaka mmoja kufuatia kuripoti juu ya kifo cha msichana Mahsa Amini aliyefariki akiwa chini ya ulinzi wa polisi ya kulinda maadili ya Iran mnamo mwezi Septemba 2022.
Hii ni hukumu ya kwanza ambayo inaweza kukatiwa rufaa ndani ya siku 20.
Soma zaidi: Tuzo ya Uhuru wa Mawazo ya Sakharov yatolewa kwa Mahsa Amini
Waandishi hao wawili: Niloufar Hamedi, aliyeripoti kwa mara ya kwanza kifo cha Mahsa Amini kwa kutojisitiri vizuri kwa kuvalia hijabu; na Elaheh Mohammadi, aliyeandika kuhusu maziko yake, walihukumiwa miaka saba na sita jela, kwa mujibu wa tovuti rasmi ya Mahakama ya Iran, Mizan.
Kulingana na tovuti hiyo, mahakama iliwatia hatiani kwa tuhuma za kushirikiana na Marekani kuyumbisha usalama wa taifa na kueneza propaganda dhidi ya mfumo wa serikali ya Kiislamu ya Iran.