1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Umoja wa Ulaya latoa tuzo kwa Mahsa Amini

Angela Mdungu
19 Oktoba 2023

Bunge la Ulaya limeitoa Tuzo ya Sakharov ya Uhuru wa Mawazo kwa Mahsa Amini, mwanamke raia wa Iran mwenye asili ya Kikurdi aliyeuwawa mikononi mwa polisi.

https://p.dw.com/p/4XlSY
Mahsa Amini
Mahsa AminiPicha: DW

Akitangaza washindi wa tuzo hiyo, Rais wa Bunge la Ulaya Roberta Metsola amesema kuwa bunge hilo linasimama na watu wenye ujasiri wanaoendelea kupambania haki sawa, utu na uhuru nchini Iran.

Metsola  alisema kuwa, mauaji ya kikatili ya Jina Mahsa Amini  aliyekuwa na miaka 22 yalikuwa ishara ya mabadiliko na kuwa  yamechochea vuguvugu linaloongozwa na wanawake linaloweka historia.

Soma zaidi: Bunge la Ulaya lamtunuku Mahsa Amini tuzo ya Uhuru ya Sakharov

Mahsa Amini, alikufa baada ya kukamatwa na polisi wa maadili wa Iran kwa tuhuma za kukiuka kanuni za mavazi  za Kiislamu. Kifo chake kilichochea maandamano makubwa nchini humo ambayo yalikandamizwa na utawala wa Tehran.

Soma zaidi: Daktari wa Congo akabidhiwa tuzo ya Sakharov

Wengine walioingia katika fainali ya tuzo hizo mwaka huu ni pamoja na Vilma Núñez de Escorcia na Askofu wa Kanisa Katoliki Rolando Álvarez  ambao wamekuwa alama muhimu katika kulinda haki za binadamu wa Nicaragua. Wengine ni wanawake watatu wa nchi za Poland, El Salvador  na Marekani wanaoongoza kupambania uavyaji mimba huru, salama na unaofuata sheria.

Tuzo ya Uhuru wa Mawazo ya Sakharov ilianza kutolewa mwaka 1988

Umoja wa Ulaya mara kwa mara umeiwekea vikwazo Iran kutokana na namna ilivyowashughulikia waandamanaji na kuwakamata.

Tuzo ya Uhuru wa Mawazo ya Sakharov imekuwa ikitolewa na Bunge la Ulaya tangu mwaka 1988 kwa watu au mashirika yanayotetea haki za binadamu na uhuru wa kujieleza.

Maandamano ya Iran yaliyofanyika baada ya kifo cha Mahsa Amini
Maandamano ya Iran yaliyofanyika baada ya kifo cha Mahsa AminiPicha: UGC/AP Photo/picture alliance

Mwaka uliopita, tuzo hiyo ilitolewa kwa watu wa Ukraine kwa mapambano yao dhidi ya uvamizi wa Urusi nchini mwao. Hafla ya kukabidhi tuzo hiyo kwa mwaka huu imepangwa kufanyika mwezi Desemba.

Tuzo ya hiyo ya  Umoja wa Ulaya ya Uhuru wa Mawazo ilipewa jina mshindi wa tuzo ya amani ya Nobeli wa Urusi Andrei Sakharov aliyepambania haki za binadamu uhuru na mabadiliko katika utawala wa Kisovieti.