Malala atuzwa tuzo ya Ulaya ya Sakharov
10 Oktoba 2013Viongozi wa kisiasa wa kundi la bunge hilo wamefanya uteuzi huo siku moja kabla ya kutangazwa tuzo ya amani ya Nobel , ambapo msichana huyo mwenye umri wa miaka 16 pia ameteuliwa kuwania tuzo hiyo.
Rais wa bunge la Ulaya Martin Schulz amesema kuwa tuzo hiyo inatambua " nguvu ya ajabu aliyonayo msichana huyo." "Malala alisimama kishujaa kutetea haki ya watoto wote kupatiwa elimu sawa. Haki hii kwa wasichana mara nyingi inatelekezwa," Schulz amesema , akidokeza kuwa "bado maisha yake yako hatarini nchini Pakistan." Schulz ameongeza.
"Nauona kuwa ni uamuzi sahihi , kwasababu yeye ni alama ya nuru kwa watu wazima wengi na ningetaraji kuwa ujasiri aliouonesha Malala siku ile unapatikana pia kwa wasichana na watoto wote duniani."
Alama ya haki
Zehra Arshad , ambaye anaongoza muungano nchini Pakistan kwa ajili ya elimu, amesema kuwa Malala "amekuwa alama ya haki ya elimu kwa kila mtoto duniani kote".
"Kuna wasichana kadha ambao wako tayari kuwa sehemu ya msafara alioanzisha Malala. Sasa ni jukumu la serikali kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa watoto wanapata elimu bora," amesema Arshad.
Mwaka mmoja uliopita wiki kama hii, Mtaliban mwenye silaha alimpiga risasi Malala kichwani akiwa katika basi la shule la wasichana katika eneo la bonde la Swat nchini Pakistan. Alifanyiwa upasuaji mjini Birmingham nchini Uingereza , ambako anaishi hivi sasa na familia yake.
Ni mshumaa unaowaka
Viongozi wa vyama vya kisiasa katika bara la Ulaya walimmiminia sifa msichana huyo , ambaye ni mtu mwenye umri mdogo kabisa kuwahi kupewa tuzo hiyo ya Sakharov.
"Malala anakuwa alama ya vita ya kudai elimu kwa wasichana katika maeneo ambako heshima kwa wanawake na haki zao za msingi zinapuuzwa kabisa, " amesema mbunge wa bunge la Ulaya Joseph Daul, ambaye ni mwenyekiti wa chama cha European Peoples Party, ikiwa ni kundi kubwa katika bunge la Ulaya.
"Yeye ni taswira ya ukakamavu kwa vijana wote ambao wanaweza kujaribu kufuata matakwa yao na, kama mshumaa, analeta nuru katika njia iliyokuwa na giza," ameongeza Daul.
"Ni upuuzi kuwa leo hii wanawake na wasichana bado wanahitaji kupambana kwa ajili ya kutafuta usawa na elimu," amesema mbunge wa Umoja wa Ulaya Nannes Swoboda, kiongozi wa Wasoshalist na Wademocrats. " Katika mapambano haya , watu binafsi kama Malala ni muhimu sana, " amesema mbunge huyo.
Wakati huo huo kundi la Taliban la Pakistan limesema leo kuwa msichana huyo Malala hajafanya lolote kuweza kustahili tuzo ya heshima ya Umoja wa Ulaya na kusema wataendelea na juhudi zao za kutaka kumuua.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / ape
Mhariri : Yusuf , Saumu