India yaweka vizuizi baada ya kirusi cha Nipah kuuwa watu 2
14 Septemba 2023Wahudumu wa afya 153 wako chini ya uangalizi baada ya kujihusisha na watu waliopata maambukizi hayo.
India imezuia mikusanyiko ya watu na kufunga baadhi ya shule katika jimbo la kusini la Kerala baada ya watu wawili kufariki kwa ugonjwa unaosababishwa na kirusi cha Nipah.
Virusi hivyo vinavyotajwa kutoka kwapopo au nguruwe husababisha homa kali, kutapika, kushindwa kupumua na hata kusababisha ugonjwa wa kupooza.
Watu watatu wamegundulika kuambukizwa virusi hivyo huku zaidi ya watu 700 wakiwemo wafanyakazi wa afya 153 ambao waliwahudumia watu hao walioambukizwa wakitengwa kwa ajili ya uangalizi zaidi.
Wakati watu hao waliofanyiwa vipimo wakisubiria majibu ya vipimo vyao, mamlaka katika eneo hilo la kusini mwa India inatarajiwa kufanya vipimo kwa watu wengi zaidi ili kubaini ukubwa na kasi ya kusambaa kwa virusi hivyo ambavyo hadi sasa vimeleta taharuki miongoni mwa watu nchini India.
Kiongozi Mkuu wa jimbo la Karela, Pinarayi Vijayan amewaamuru watu katika jimbo hilo hasa katika wilaya ya Kozhikode kuepuka mikusanyiko isiyo na ulazima kwa angalau siku 10 ili kupunguza kasi ya maambukizi.
WHO: Yazungumzia virusi hivyo hatari
Shirika la Afya duniani WHO linaeleza kwamba virusi hivi hatari vya Nipah vinaambukizwa kutoka kwa wanyama kama nguruwe na popo na kuenezwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine.
Dalili za awali zinajidhihirisha baada ya siku nne hadi kumi na nne baada ya maambukizi.
WHO inasema wakati mwingine inaweza kuchukua muda mrefu wa hadi siku 45.
Mwaka 2018, watu wasiopungua 17 walikufa baada ya kuambukizwa na virusi hivyo huko Kerala nchini India.
Soma pia:WHO kujadili kitisho cha UVIKO-19
Jimbo jirani la Tamil Nadu limetangaza kuwa wasafiri wanaotokea katika jimbo la Kerala watalazimika kufanyiwa vipimo vya afya na wale watakaobainika kuwa na maambukizi watalazimika kujitenga kwa muda.
Virusi hivyo vilitambuliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1998 baada ya kusambaa miongoni mwa wafugaji wa nguruwe nchini Malaysia.
Huko India, mlipuko wa kwanza wa Nipah uliripotiwa katika jimbo la West Bengal mnamo 2001.
Shirika la Afya Duniani WHO limeorodhesha virusi vya Nipah kama ugonjwa hatari zaidi kwa umma.
Imeinywa kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kuwa janga kubwa kwa kuwa bado hakuna njia za kutosha za kuweza kuukabili.