1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAsia

WHO ina wasiwasi juu ya kuongezeka kwa UVIKO-19 China

5 Januari 2023

Mkuu wa WHO amesema shirika hilo "lina wasiwasi juu ya hatari ya maisha China" katika wakati mripuko wa virusi vya corona unaenea kote nchini humo na kuna ukosefu wa takwimu za uhakika kutoka kwa serikali ya Beijing.

https://p.dw.com/p/4Ll62
Mehr Länder führen Corona-Testpflicht für Reisende aus China ein
Picha: Alessandra Tarantino/AP Photo/picture alliance

Mkurugenzi wa shirika la afya duniani Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema hivi karibuni walikutana na maafisa wa China ili kusisitiza umuhimu wa Beijing kuweka wazi takwimu na taarifa zote za masuala ya Uviko-19 ikiwa ni pamoja idadi ya watu wanaolazwa hospitalini na aina ya virusi hata kama janga hilo linaendelea kupungua kimataifa tangu lilipoanza mwishoni mwa 2019.

Mkurugenzi wa dharura wa WHO Michael Ryan aliwaambia waandishi wa habari jana Jumatano kwamba takwimu rasmi za China hazionyeshi athari halisi ya mlipuko huo ambapo visa vya maambukizo vimeongezeka baada ya uamuzi wa Beijing mwezi uliopita wa kuondoa ghafla udhibiti mkali wa UVIKO-19

Hii leo China imejibu kauli hiyo kwa kutoa wito kwa WHO kuchukua msimamo "sawa" juu ya UVIKO-19, kwa kusema kwamba "inadumisha ushirikiano wa karibu na WHO" na kwamba daima ilikuwa ikikabidhi taarifa na takwimu muhimu kwa jumuiya ya kimataifa, kwa njia za uwazi".