China yaiomba Ulaya kulitathmini janga la UVIKO-19 kwa haki
6 Januari 2023China imeutaka Umoja wa Ulaya kufanya tathmini ya haki kuhusu janga la Corona nchini humo. Kauli hiyo imefuatia hatua za maafisa wa serikali za Umoja wa Ulaya kupendekeza kwamba wasafiri wote wanaoingia kutoka China wanatakiwa kuthibitisha kwamba hawana maambukizo ya UVIKO-19 kabla ya kuanza safari.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China, Mao Ning, amesema Umoja wa Ulaya unapaswa kuzingatia kwa haki hali ya janga la UVIKO-19. Ning ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi habari mjini Beijing.
Ujerumani, Ubelgiji, Sweden na Ugiriki zilitangaza jana Alhamisi kuakianzisha upimaji wa lazima wa virusi vya korona kwa wasafiri kutoka China wakifuatilia maagizo ya wataalam wa afya mjini Brussels.
Soma Zaidi: EU yachukua hatua kufuatia mlipuko wa UVIKO-19, China
Nchi hizo nne zilichukua hatua baada ya Uingereza, Ufaransa, Italia, Korea ya Kusini na Marekani hapo awali kutangaza masharti ya ziada kwa wasafiri kutoka China. Kulingana na kituo cha habari cha ERT, wasafiri kutoka China watalazimika kuthibitisha kwamba hawana korona kabla ya kuingia nchini Ugiriki.
Kwa upande wake, waziri wa Afya wa Ujerumani, Karl Lauterbach, alisema kanuni za kuingia Ujerumani zitabadilishwa kwa muda mfupi na kwamba wasafiri kutoka China katika siku zijazo watahitaji angalau vipimo vya haraka vya korona wakati wa kuingia Ujerumani. Haikuwa wazi mara moja ni lini hatua mpya zitaanza kutumika.
Waziri wa afya wa Ufaransa, Francois Braun, amesema, "Nchini Ufaransa, idadi ya visa vya korona kwa sasa inapungua sana, pamoja na suala la kulazwa hospitalini. Lakini kinachotokea China kinatia wasiwasi, na hii ndiyo sababu ya hatua ambazo waziri mkuu na mimi tumechukua katika agizo la ukaguzi kwa wasafiri wanaofika kutoka China.''
Jumatano, wataalam wa afya wa Umoja wa Ulaya walishindwa kukubaliana juu ya vipimo vya lazima kwa wasafiri kutoka China, lakini walitoa pendekezo kali badala yake. Wataalam pia walishauri kwamba abiria ndani ya ndege kutoka China wanapaswa kuvaa barakoa ya aina ya FFP2 au N95.
Mkutano huo wa Brussels ulikuja wakati virusi vikienea kwa kasi nchini China, ambapo mamlaka ilitupilia mbali sera yake ya kupambana na UVIKO-19 ambayo ilihusika na kuweka vizuizi vikali, vipimo vya wingi na kuwekwa karantini kwa lazima kwa karibu miaka mitatu. Hatua hiyo ilizua wimbi la maambukizo ambayo nchi hiyo hazijawahi kushuhudia.
Haijulikani hata hivyo ikiwa idadi ya visa vya maambukizio nchini China itakuwa na athari katika nchi za Umoja wa Ulaya. Aina mpya ya kirusi cha China tayari kimezunguka katika nchi za Umoja wa Ulaya na wataalamu wamesema hakija sababisha changamoto kwa mfumo wa kinga kwa raia katika umoja huo.
Sikiliza Zaidi: