Ulaya na mkakati wa kuwapima UVIKO-19 abiria kutoka China
4 Januari 2023Mataifa hayo yanazingatia kuweka vizuizi vya safari ambavyo vinaweza kuikasirisha China na sekta ya usafiri wa anga duniani.
Mapema Jumatano, Tim McPhie, msemaji wa Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na masuala ya Afya, Stella Kyriakides, amesema nchi nyingi za umoja huo zinaunga mkono hatua ya kuweka masharti ya kuwapima kwa lazima abiria kutoka China virusi vya corona kabla ya kuondoka.
''Mazungumzo ya leo yataangazia hali ya mripuko na yatalenga kuweka msimamo wa pamoja wa Umoja wa Ulaya kuhusu hatua zinazoweza kuchukuliwa. Sasa hatua hizi zinalingana na zile zilizowekwa na Kamishna Kyriakides, katika barua ambayo aliwatumia mawaziri wa afya baada ya mkutano wa Desemba 29,'' alifafanua McPhie.
China yatishia kuchukua hatua
China tayari imekosoa vikali vizuizi vya usafiri ambavyo baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya imeanza kuviweka, na imeonya itachukua hatua za kukabiliana navyo katika siku zijazo.
Serikali ya China na wataalamu wa afya wa Umoja wa Ulaya wamesema hakuna haja kubwa ya kuweka vikwazo vyovyote vya usafiri kwa kuwa aina ya virusi vya corona vinavyoibuka kutoka China, tayari vimeenea Ulaya.
Siku ya Jumatano, Chama cha Kimataifa cha Usafiri wa Anga, IATA ambacho kinajumuisha mashirika 300 ya ndege duniani kote, kimeelezea kupinga hatua ya kuwekwa vizuizi vya usafiri wa anga.
Mkurugenzi Mkuu wa IATA, Willie Walsh amesema utafiti uliofanywa kuhusu kirusi aina ya Omicron unahitimisha kwamba kuweka vizuizi katika usafiri wa anga hakutoleta tofauti yoyote katika kuzuia kuenea kwa maambukizi.
Msemaji wa Serikali ya China, Mao Ning amesema leo kuwa wana matumaini kwamba pande zote zitazingatia kupambana na janga lenyewe, na kuepuka siasa za UVIKO-19.
Dhamira ya Ulaya kuchukua hatua za pamoja
Hata hivyo, bado Umoja wa Ulaya umeonyesha dhamira yake ya kuchukua hatua za pamoja kuhakikisha abiria wanaoingia kutoka China hawawezi kwa namna yoyote ile kusambaza virusi vipya barani humo.
Sweden, ambayo ndiyo inashikilia urais wa Umoja wa Ulaya kwa sasa, imesema wasafiri kutoka China wanahitaji kujiandaa kwa maamuzi yatakayochukuliwa katika muda mfupi.
Pamoja na kupima virusi vya corona kabla ya kusafiri, mataifa ya Umoja wa Ulaya huenda yakakubaliana kuhusu upimaji maalum wa maji machafu katika ndege zinazoingia kutoka China, kuona iwapo yana aina hatari ya virusi ambavyo bado sio vya kawaida katika bara la Ulaya.
Italia ilikuwa nchi ya kwanza mwanachama wa Umoja wa Ulaya kuhitaji vipimo vya virusi vya corona kwa abiria wa ndege wnaoingia kutoka China, lakini Ufaransa na Uhispania zilifuata mara moja hatua kama hizo.
(AP, Reuters)