1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
AfyaChina

China yakosoa masharti mapya yaliotolewa kwa wasafiri wake

3 Januari 2023

China imekosoa masharti mapya ya upimaji uviko-19 yaliotolewa na mataifa kadhaa kwa abiria wanaosafiri nje kutoka eneo lake.

https://p.dw.com/p/4Lfq5
Coronavirus - China
Picha: Andy Wong/AP/dpa/picture alliance

Marekani, Canada, Ufaransa na Japan ni miongoni mwa mataifa yanayowataka sasa wasafiri kutoka China kuonesha matokeo ya vipimo yanayoonyesha hawana maambukizo ya uviko-19, kabla ya kuwasili, wakati nchi hiyo ikikabiliwa na ongezeko la visa vya maambukizo.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Mao Ning ameuambia mkutano wa kawaida wa wanahabari, kwamba maamuzi ya mataifa hayo hayakubaliki.

''Tuko tayari kuboresha mawasiliano na dunia na kufanyakazi pamoja ili kuvuka janga la Uviko-19. Lakini pia tunaamini kwamba masharti yaliowekwa na mataifa dhidi ya China pekee yake yanakosa msingi wa Kisayansi, baadhi ya matendo yaliopitiliza hayakubaliki kabisaa.''

Mwishoni mwa Desemba, China ilisema wasafiri wanaoingia nchini humo hawatahitaji tena kukaa karantini.

Mataifa yalioweka masharti yametaja ukosefu wa uwazi wa China kuhusu taarifa za ugonjwa huo na hatari ya kuibuka kwa aina mpya ya virusi kama sababu za kuweka masharti hayo.