ICJ yaiamuru Uganda kulipia DRC fidia kwa vita mkoani Ituri
10 Februari 2022Hukumu hiyo ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ, imekuja kama pigo kwa Congo, ambayo ilitaka kulipwa kiasi kikubwa zaidi cha dola bilioni 11, kama fidia ya vita hivyo vilivyodumu kuanzia mwaka 1998 hadi 2003.
Kesi hiyo iliyodumu kwa muda mrefu zaidi katika mahakama ya Umoja wa Mataifa ICJ inayotatua mizozo baina ya mataifa, yenye makao yake mjini The Hague, imemalizika kwa jaji kuiamuru Uganda kulipa fidia kwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, kutokana na ghasia na madhara iliyoyapata, lakini haikufikia madai ya DRC ya dola bilioni 11.
Soma pia: Uganda kuilipa DRC zaidi ya dola bilioni 11?
Kiwango hicho ambacho Uganda imeamuriwa kulipa, kitalipwa kwa awamu, za dola milioni 65 kwa kipindi cha miaka mitano. Uganda imesema hata hivyo kuwa hukumu hiyo siyo ya haki na ni makosa.
Wakati kiasi kilichotolewa ni kidogo sana kuliko kilichotakiwa na DRC, Uganda bado inaichukulia hukumu hiyo kutokuwa ya haki na ya makosa, kama ilivyokuwa kwa hukumu iliyopita mwaka 2005," alisema wizara ya mambo ya nje katika taarifa.
Wakati Majaji wamethibitisha kwamba Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ilidhulumiwa katika vita ya mkoa wa Ituri miongo miwili iliyopita, waliweka wazi pia kwamba mataifa hayo jirani yangeweza kufikia muafaka kuhusu athari za vita hiyo.
Dhulma za kihistoria
Kesi hiyo ilianza kwa shauri lililofunguliwa na DRC mwaka 1999, ambalo awali ilielekezwa dhidi ya mataifa jirani ya Uganda, Burundi na Rwanda.
Serikali ya Congo iliyashutumu mataifa hayo kwa "ukiukaji wa wazi" wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kwa sababu wanajeshi kutoka mataifa hayo yaliingilia vita vya kuwania mkoa wenye utajiri wa rasilimali wa Ituri na kuunga mkono wanamgambo mbalimbali huko kwa maslahi yao binafsi, ingawa Kinshasa iliondoa idhini yake kwao kufanya baada ya awali kuyaruhusu.
Soma pia: Uganda yasema hukumu ya ICJ haikuwa ya haki na isiyostahiki
Baada ya miaka kadhaa ya mabishano, Uganda iliachwa kama mshtakiwa.
Na mwaka 2005, mahakama hiyo ilitoa hukumu ngumu ya kihistoria ambayo ilielezea kwamba Uganda iliua raia, kushindwa kutofautisha kati ya maeneo ya kijeshi na kiraia, ilishindwa kuwalinda raia dhidi ya wapiganaji, na kama taifa la ukaliaji, ilishindwa kuchukuwa hatua kulinda haki za biandamu na kutekeleza sheria ya kimataifa. Hukumu hii iliweka msingi wa madai ya DRC kuhusu fidia, kutokana mzozo huo mbaya wa kivita.
Hata hivyo mahakama hiyo pia ilizitaka pande mbili kwenye mzozo huo kukubaliana juu ya kiwango cha fidia. Hili lilidhihirika kutowezekana hata hivyo, kwa sababu serikali ya Congo iliweka kiwango cha uharibifu iliyoupata kuwa dola bilioni 11.
Soma pia: Mahakama ya UN yaipa ushindi Qatar kesi ya kufungiwa anga
Uganda ilikataa kiwango hicho, ikikitaja kuwa cha kuharibu na kilichonuwia kuua uchumi wake. Kesi hiyo ilirejeshwa katika mahakama ya The Hague, ambayo sasa ilibidi kuamua swali gumu la ni kiasi gani kingefaa kwa vifo na uharibifu mwingine wa vita vya Ituri.
Kimsingi, fidia hailengi kumuadhibu adui, bali kulipia makosa yaliotendeka, kwa mujibu wa sababu za hukumu hiyo, iliyosomwa na Jaji mkuu Joan Donoghue.
Mwishowe, Jaji huyo alitangaza kiwango cha kulipwa kuwa dola milioni 325, zikijumlisha dola milioni 225 kwa vifo na majeraha, dola milioni 40 kwa uharibifu wa mali, na dola milioni 60 kwa wizi wa rasilimali, ukataji wa misitu na ujangili.