1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda yasema hukumu ya ICJ haikuwa ya haki na isiyostahiki

10 Februari 2022

Uganda imesema hii leo kwamba inaichukulia hukumu ya mahakama ya kimataifa ya haki, ICJ iliyoitaka kuilipa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo dola milioni 325, kuwa isiyo ya haki na isiyostahiki.

https://p.dw.com/p/46nxX
Den Haag Internationaler Gerichtshof ICJ Entscheidung Bolivien Chile
Picha: Getty Images/AFP/J. Lampen

Uganda imetakiwa kuilipa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuhusiana na wajibu wake katika mizozo kwenye jimbo lenye utajiri wa rasilimali la Ituri.

Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Uganda imesema ingawa kiwango kilichotajwa kwenye hukumu hiyo ni kidogo mno ikilinganishwa na kile kilichotarajiwa, Uganda pia inaiona hukumu hiyo kuwa isiyo sawa na mbaya, kama tu ilivyokuwa kwenye hukumu ya awali ya mwaka 2005.  

Hukumu hiyo ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ, imekuja kama pigo kwa Congo, ambayo ilitaka kulipwa kiasi kikubwa zaidi cha dola bilioni 11, kama fidia ya vita hivyo vilivyodumu kuanzia mwaka 1998 hadi 2003.

Kesi hiyo ilianza kwa shauri lililofunguliwa na DRC mwaka 1999, ambalo awali ilielekezwa dhidi ya mataifa jirani ya Uganda, Burundi na Rwanda.

Serikali ya Congo iliyashutumu mataifa hayo kwa "ukiukaji wa wazi" wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kwa sababu wanajeshi kutoka mataifa hayo yaliingilia vita vya kuwania mkoa wenye utajiri wa rasilimali wa Ituri na kuunga mkono wanamgambo mbalimbali huko kwa maslahi yao binafsi.