1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya Usalama yazidi kuzorota Somalia

23 Septemba 2010

Hali inatisha nchini Somalia baada ya mapambano kati ya vikosi vya Umoja wa Afrika na wanamgambo wa Al Shabab katika soko la Bakara, ambayo yamegharimu maisha ya watu wapatao 20.

https://p.dw.com/p/PL7g
Wanamgambo wa itikadi kali-al Shabab wapiga doria mjini MogadischoPicha: AP

Inawezekana wakati Waziri Mkuu Omar Abdirashid Ali Sharmarke anajiuzulu mwanzoni mwa wiki hii, hakuwa na tena cha kufanya kuyanusuru madaraka yake wala kuizamua nchi yake kutoka dimbwi la machafuko na hali ya kutokuaminiana. Mgogoro wake na Rais Sheikh Sharif Sheikh Ahmed ni kielelezo tu cha ugomvi na mgogoro unaoiandama na kuiangamiza jamii ya Kisomali kwa miongo zaidi ya miwili sasa.

Matokeo ya kutokufahamiana huko, ndio mashambulizi kama ya leo yaliyotokea kwenye eneo la soko la Bakara, mjini Mogadisho, ambayo hadi sasa yameshagharimu roho 20 za Wasomali, kwa mujibu vyanzo vya kitabibu nchini humo. Mkuu wa Huduma za Dharura wa Mogadisho, Ali Muse, ameliambia Shirika la Habari la Ujerumani, DPA, kwamba haya ni maafa makubwa kutokea katika miezi ya karibuni.

Mauaji haya yamesababishwa na mashambulizi yaliyofanywa na vikosi vya serikali vinavyosaidiwa na wanajeshi wa Umoja wa Afrika. Eneo la Bakara ni ngome ya wapiganaji wa Al Shabbaab, ambao wanamiliki sehemu kubwa ya Kusini na Kaskazini ya mji wa Mogadisho. Kwa miezi ya karibuni, Al Shabbaab wamejizatiti kuongeza eneo lao la udhibiti wa nchi hiyo, ili kuweka utawala wa Kiislam. Tayari wapiganaji hao wanashikilia sehemu kubwa ya nchi, huku serikali dhaifu ya Sheikh Sharif ikidhibiti sehemu ndogo tu ya mji wa Mogadisho.

Somalia Mogadischu Islamisten Flüchtlinge
Majeruhi anapelekwa hospitali mjini MogadishoPicha: AP

Tangu ilipopinduliwa serikali ya kidikteta ya Rais Siyad Baree hapo mwaka 1991, Somalia imekuwa haina serikali yenye mamlaka nchi nzima. Tangu hapo, mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, yaliyoanza kwa sura ya koo na kikabila, yamekuwa yakiangamiza maelfu ya raia wa nchi hiyo, yakizalisha wakimbizi na yakiusambaratisha kabisa uchumi.

Sasa mapigano yamechukuwa sura ya imani za kisiasa, baina ya Al Shabbaab, wanaoaminika kuwa na msimamo mkali wa kidini na kuungwa mkono na Al Qaeda, na Serikali legelege inayoambiwa inaongozwa na watu msimamo wa wastani na wanaoungwa mkono na nchi za Magharibi na Umoja wa Afrika. Kwa miaka mitatu tu iliyopita, mapigano haya yameshagharimu maisha ya zaidi ya watu 21,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto. Kwa kiasi kikubwa, mauaji yanayotokea nchini Somalia hufanywa kwa raia wasiokuwa na hatia.

Makundi ya haki za binaadamu yanazilaumu pande zote zinazoshiriki kwenye mapigano haya kwa kuelekeza mashambulizi yao kwenye maeneo ya kiraia. Na ingawa kikosi cha AMISOM, kimekuwa kila mara kikisisitiza kufanya kila liwezekanalo kuepusha maafa kwa raia, ukweli unabakia kwamba, wanaoumizwa zaidi na mapigano haya si wanamgambo wa Al Shabbaab, ambao kila siku wamekuwa wakijidhibiti kufanya mashambulizi mapya.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DAP/AFP


Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman