Al Shabab kulipiza kisasi kifo cha Nabhan
16 Septemba 2009Operesheni hiyo ilifanyika eneo la kusini mwa Somalia.Kufuatia tukio hilo kundi hilo limewatolea wito wapiganaji wa makundi mengine ya kigeni kuwaunga mkono.Kwa upande mwengine kundi Al Shabab limeweka nadhiri litalipiza kisasi baada ya kamanda wao kuuawa na wanajeshi wa Marekani.
Kundi la Al Shabab lililo na mafungamano na kundi la kigaidi la Al Qaeda limekiri kuwa kamanda wao mmoja wa ngazi za juu aliuawa katika operesheni ya Marekani iliyofanyika mwanzoni mwa wiki hii.Maafisa wa serikali wa Marekani wamethibitisha kuwa shambulio hilo lilifanyika na kamanda Saleh Ali Saleh Nabhan aliuawa katika operesheni hiyo.Nabhan ni raia wa Kenya anayesakwa na shirika la ujasusi la Marekani FBI kwasababu ya tuhuma za kuhusika mwaka 2002 katika shambulio dhidi ya hoteli moja ya Waisraeli pamoja na jaribio la kuilipua ndege ya Israel iliyokuwa ikijiandaa kuondoka katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mombasa.
Operesheni ya helikopta sita
Kwa mujibu wa mtandao wa shirika la Global Islamic Media Front,kundi la Al Shabab lilichapisha taarifa iliyoeleza kuwa helikopta sita zilitumiwa katika shambulio hilo na likalilipua gari walimokuwa wakisafiria wapiganaji hao. Kulingana na wadadisi shambulio hilo lilifanikiwa ila huenda likawaghadhabisha zaidi wapiganaji hao.
Kwa upande mwengine kamanda mmoja wa ngazi za juu wa kundi la Al Shabab aliyezungumza na shirika la habari la AFP alisema kuwa watalipiza kisasi kufuatia shambulio hilo.
Gavana wa eneo la Lower Shabelle kulikotokea shambulio hilo amesema kuwa raia watatu wa kawaida nao pia waliuawa katika shambulio hilo japo maelezo kamili bado hayajapatikana.Maiti ya Nabhan Iko mikononi mwa wanajeshi wa Marekani kwa lengo la kuichunguza ili kuhakikisha kuwa ni yule wanayemsaka.
Kuweka nadhiri
Wakati huohuo Kundi la Al-Shabab limewatolea wito wapiganaji wengine wa kigeni kuwaunga mkono nchini Somalia kufuatia shambulio hilo. Akizungumza na waandishi wa habari kamanda wa kundi hilo katika maeneo ya Bay na Bakol aliwatolea wito wapiganaji wa kiislamu kutoka sehemu zote za ulimwengu kuwaunga mkono huko Somalia.Kamanda huyo alihoji kuwa ikiwa vikosi vy akulinda amani vya Umoja wa Afrika kutoka mataifa ya Burundi na Uganda ambao si waislamu wanaruhusiwa kuwa Somalia kwanini wapiganaji wa kiislamu wasiingie humo?Wanajeshi hao wa Umoja wa Afrika wa kulinda amani wanaiunga mkono serikali ya Somalia.Wanajeshi wa Marejani wameebadili mbinu zao kwa kufanya mashambulizi ya helikopta badala ya kulipua mabomu ili kuwasaka wapiganaji wa Somalia.Kulingana na mashirika ya usalama ya mataifa ya magharibi Somalia imekuwa mahala salama pa wapiganaji kujificha wakiwemo pia wale walio na misimamo mikali wanaolitumia eneo hilo kupanga njama za mashambulizi katika maeneo mengine ya ulimwengu.Kauli hizo zinaungwa mkono na Rashid Abdi mtaalam wa masuala ya Somalia katika shirika la International Crisis Group anayetoa onyo,''Kwamba kundi la Al Shabab litatimiza tishio la kuyashambulia mataifa ya magharibi hususan marekani ni jambo ambalo marekani haipaswi kuipa uzito mdogo.''alisisitiza.
Vita nchini humo vilivyoanza tangu mwaka 2007 vimesababisha vifo vya zaidi ya raia alfu 18.
Wanajeshi wa Marekani wamekuwa wakiishambulia Somalia wakiwa na lengo la kuwasaka watuhumiwa waliohusika na shambulio dhidi ya balozi za Marekani katika miji ya Nairobi na Dar es salaam mwaka 1998.Hii ni mara ya kwanza Marekani imefanikiwa kulishambulia kundi la Al Qaeda nchini Somalia.
Mwandishi:Thelma Mwadzaya /AFPE-RTRE
Mhariri:Othman Miraji