China na Saudi Arabia wasaini makubaliano ya ushirikiano
8 Desemba 2022Rais wa China Xi Jinpingamekutana hii leo na mfalme pamoja na mwanamfalme wa Saudi Arabia akiwa ziarani kwenye taifa hilo la kifalme. Lengo la ziara hiyo ni kuimarisha mahusiano na ukanda huo muhimu kwa usambazaji wa nishati nchini mwake, katika wakati ambapo vikwazo vya nchi za magharibi dhidi ya Urusi vikizidi kuongeza ugumu katika upatikanaji wa nishati.
Mchana wa leo, rais Xi alikutana na mwanamfalme Mohammed bin Salman katika kasri la Al Yamama mjini Riyadh. Mohammed bin Salman, mwana wa mfalme Salaman ndiye anayetarajiwa kuliongoza taifa hilo tajiri wa mafuta katika kipindi cha miongo mingi ijayo.
Soma Zaidi: Rais wa China kuitembelea Saudi Arabia siku ya Jumatano
Baada ya mazungumzo, wakuu hao walisaini makubaliano muhimu na ya kimkakati ya ushirikiano, katika maeneo ya nishati ya haidrojeni na makubaliano ya kuhamasisha uwekezaji wa moja kwa moja baina ya mataifa hayo mawili hii ikiwa ni kulingana na shirika la habari la serikali, SPA mapema leo. Aidha wakuu hao wamesaini makubaliano ya kushirikiana katika utekelezaji wa maono ya mwanamfalme ya mwaka 2030 sambamba na mpango wa Beijing wa ukanda wa barabara.
Pamoja na mikataba hiyo, Saudi Arabia pia imesaini makubaliano na kampuni kubwa ya teknolojia ya China, Huawei unaojikita kwenye masuala ya teknolojia, hii ikiwa ni kulingana na ofisi ya mawasiliano ya serikali kwenye taarifa yake.
China inasema haya ni makubaliano yaliyoanza muda mrefu.
Balozi wa China nchini Saudi Arabia Chen Weiqing amesema makubaliano haya ni miongoni mwa hatua zilizoanza kuchukuliwa tangu huko nyuma wakati China ilipoanzisha mradi mkubwa wa barabara unaoiunganisha na mataifa mengi ulimwenguni.
Amesema "Makubaliano haya ya kirafiki kati ya China na Saudi Arabia yanaweza kuangaziwa tangu huko nyuma wakati tulipoanzisha mradi mkubwa wa barabara, kama miaka 100 hadi 1000 iliyopita. Nilipotembelea maktaba ya mfalme Abdulaziz, mtumishi alinionyesha ramani kutoka China. Ramani hiyo ilionyesha barabara zilizounganisha mji wa chang'an na Mecca nchini Saudi Arabia. Kwa hivyo makubaliano haya kati ya mataifa haya mawili yanaungwa mkono kwa kiasi kikubwa."
Hata hivyo haikijulikana wazi ni masuala gani hasa waliyojadiliana kwenye mazungumzo, ingawa Xi alinukuliwa kwenye safu ya maoni ya gazeti la Al Riyadh la Saudi Arabia akisema makubaliano baina ya mataifa hayo mawili yana historia ya tangu miaka 2000 iliyopita na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano na Mataifa ya Kiarabu ambayo ni pamoja na Umoja wa Falme za Kiarabu, Oman, Qatar na Bahrain na hasa katika wakati huu wa changamoto ya nishati ulimwenguni.
Mataifa ya Kiarabu yanajaribu kuziboresha upya sera zao za kigeni katika wakati ambapo Marekani imeamua kusaka washirika kutoka maeneo mengine ulimwenguni.
Vita vya Urusi nchini Ukraine na hatua kali dhidi ya Moscow vimeyasukumua mataifa ya Kiarabu kuangazia kuimarisha uhusiano na China na kwa manamfalme Mohammed, hatua hii ya kukutana na Xi inaimarisha mtizamo wake kwenye uso wa kimataifa, baada ya kuhusishwa na mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari Jamal Khasshoggi.