Rais wa China Xi Jinping azuru Saudi Arabia
7 Desemba 2022Ziara hii ya Xi Jinpinginafanyika pia baada ya miezi kadhaa ya mivutano baina yanchi hizo mbili na Marekani.
Rais Xi Jinping anatarajiwa kufanya mikutano na viongozi wa taifa hilo lenye utajiri wa mafuta na ambayo ni muhimu kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa nishati hiyo nchini mwake, wakati Beijing ikijaribu kufufua uchumi wake ulioathiriwa na hatua kali za kudhibiti kusambaa kwa virusi vya UVIKO-19.
Soma Zaidi: Rais wa China kuitembelea Saudi Arabia siku ya Jumatano
Xi aliyerejea mamlakani hivi karibuni amewasili katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh, hii ikiwa ni kulingana na vyombo vya habari vya China na Saudi Arabia tayari kwa ziara ya siku tatu ambapo atafanya mazungumzo na viongozi wa Saudi Arabia na mataifa mengine ya Kiarabu.
Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia mwanamfalme Faisal bin Farhan na gavana wa Riyadh mwanamfalme Faisal bin Bandar walikuwa miongoni mwa waliomkaribisha Xi alipowasili kwenye uwanja wa ndege.
Saudi Arabia inatarajia kuitumia ziara hiyo kujaribu kurekebisha sera zake za kigeni, wakati Marekani ikiigeuzia mgongo na kusaka washirika kwingineko ulimwenguni, huku vita vya Urusi nchini Ukraine na misimamo mikali ya magharibi dhidi ya Moscow pia vikilisukuma taifa hilo la Kiarabu kuangazia kuimarisha mahusiano na China
Msemaji wa mambo ya nje wa China Mao Ning alisema, "Ushirikiano kati ya nchi husika unapaswa kuleta amani na utulivu wa kikanda. Marekani imeunda ushirikiano wa kijeshi na baadhi ya washirika wake ili kuibua migawanyiko na makabiliano na kudhoofisha amani na utulivu wa kikanda. Haifai na haitupeleki popote."
Ning amesema rais Xi atahudhuria ufunguzi wa mkutano wa kilele wa China na ushirikiano wa Mataifa ya Kiarabu, GCC. Mkutano huo unaotajwa kama jukwaa la ngazi za juu kabisa la kidiplomasia baina ya mataifa hayo, ni wa kwanza kuwahi kufanyika tangu kuasisiwa kwa Jamhuri ya Watu wa China.
Ameongeza kuwa mkutano huo aidha utakuwa ni hatua kubwa ya kihistoria katika mahusiano ya kimaendeleo kati ya China na mataifa ya yaliyoko kwenye ushirikiano huo ambayo ni pamoja na Bahrain, Kuwait, Oman, Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Xi anapanga kukutana na mfalme Salman wa Saudi Arabia pamoja na mwanamfalme Mohammed bin Salman. Kwa mwanamfalme, hii ni hatua kubwa ya kujiimarisha katika jukwaa la kimataifa na hasa baada ya kuhusishwa na mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa Saudi Arabia Jamal Khashoggi.
China ni mnunuzi mkubwa wa mafuta kutoka Saudi Arabia na kwa pamoja wanaonekana kuwa na shauku ya kupanua mahusiano yao katika wakati ambapo kunashuhudiwa mzozo wa kiuchumi na mabadiliko ya siasa za kimaeneo.
Hata hivyo, Marekani kupitia msemaji wa Ikulu ya White House John Kirby imeikosoa ziara hiyo ya Xi ikisema ni mfano wa majaribio ya China ya kupanua ushawishi wake ulimwenguni, lakini hautabadilisha sera zake kuelekea Mashariki ya Kati.