1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brahimi ateuliwa mpatanishi mpya kuhusu Syria

18 Agosti 2012

Mwanadiplomasia mzoefu wa Algeria, Lakhdar Brahimi ameteuliwa na Umoja wa Mataifa kuwa mpatanishi mpya wa kimataifa katika mgogoro wa Syria, akichukua nafasi ya Kofi Annan alieamua kutoendelea na majukumu hayo.

https://p.dw.com/p/15sEo
Lakhdar Brahimi, mpatanishi mpya katika mgogoro wa Syria
Lakhdar Brahimi, mpatanishi mpya katika mgogoro wa SyriaPicha: dapd

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amezitaka nchi zenye nguvu duniani kumuunga mkono mpatanishi huyo mpya. Hata hivyo, Lakhdar Brahimi amekwishasema kuwa hana imani kubwa kuwa ataweza kuusuluhisha mgogoro wa Syria, ambao umekuwepo kwa muda wa miezi 17.

Mtangulizi wa Brahimi, Katibu Mkuu wa Zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan atamaliza muda wake wa upatanishi mwishoni mwa mwezi huu wa Agosti, na alikataa kuongezewa muda akisema jumuiya ya kimataifa haikumuunga mkono vya kutosha, katika juhudi zake za kuitaka serikali ya rais Bashar al-Assad na waasi kusuluhisha tofauti zao.

Kofi Annan, mpatanishi wa kwanza katika mgogoro wa Libya anayeondoka
Kofi Annan, mpatanishi wa kwanza katika mgogoro wa Libya anayeondokaPicha: Reuters

Mwanadiplomasia mahiri

Mpatanishi mpya, Lakhdar Brahimi mwenye umri wa miaka 78, alikuwa waziri wa mambo ya nchi za Algeria kati ya mwaka 1991 na 1993 na alikuwa mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan kabla ya vita vilivyofuatia mashambulizi ya Septemba 11, 2001 nchini Marekani, na nchini Irak baada ya vita vya mwaka 2003.

Brahimi pia alikuwa mjumbe wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu katika mzozo wa Lebanon, na aliweza kupata suluhu kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo mwaka 1980, kwa kufanya mazungumzo na serikali ya Syria wakati huo.

Naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa Eduardo del Buey amesema Brahimi atawasili mjini New York hivi karibuni kwa mashauriano. Amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Lakhdar Brahimi kwa utayarifu aliouonyesha, kutaka kutumia kipawa chake na uzoefu wa muda mrefu katika kujaribu kuupatia suluhu mgogoro mkubwa wa Syria.

Ban Ki-moon ampigia debe Brahimi

Ban Ki-moon pia amesema Umoja wa wa Mataifa , na hususan Baraza la Usalama la Umoja huo, vyapaswa kumuunga mkono kwa dhati mpatanishi huyo. Brahimi amerejelea umuhimu wa nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuzungumza kwa sauti moja kuhusu mgogoro wa Syria.

Unterschrift: UN-Generalsekretär Ban Ki Moon spricht im Parlament von Bosnien und Herzegowina (Sarajevo, 25.7.2012); Copyright: DW/Samir Huseinovic
Ban Ki Moon Parlament BosnienPicha: DW

''Wameniomba kuifanya kazi hii, lakini iwapo hawataniunga mkono, nitakuwa sina kazi ya kufanya'', alisema Brahimi na kuongeza kwamba atataka kufanya mazungumzo ya kina na baraza la Umoja wa Mataifa.

Na alipoulizwa iwapo anayo matumaini kwamba ataweza kusimamisha vita vya wenyewe nchini Syria, Lakhdar Brahimi alisema imani hana, ila atafanya kila linalowezekana.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeahidi kumuunga mkono mwakilishi mpya wa kimataifa kuhusu Syria. Pamoja na hayo lakini, kumejitokeza mgawanyiko katika baraza hilo, baada ya nchi za magharibi na za kiarabu kususia mkutano uliotishwa na Urusi kuhusu mgogoro wa Syria, na kuilazimisha Urusi kuahirisha mkutano huo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP

Mhariri: Stumai George