Muda wa ujumbe wa uangalizi Syria wamalizika
17 Agosti 2012Pamoja na hayo umoja wa mataifa ulimtangaza rasmi Lakhdar Brahimi kuwa mwanadiplomasia atakayeshughulikia mzozo wa Syria akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Kofi Annan. Masharti ya utendaji wake wa kazi hata hivyo yanaendelea kuwa magumu.
Urusi ilipendelea sana, ujumbe huo wa uchunguzi urefushiwe muda wake kwa mara nyingine, hatimaye lakini mwishowe ilikubali kushindwa. Azimio la Urusi halikuweza kupata muungaji mkono katika baraza la usalama. Balozi wa Urusi katika umoja wa mataifa Vitali Churkin hakuweza kulizuwia kundi kubwa la wajumbe wa baraza la usalama, kwa kuwa nchi hizi hazijaonyesha hatua ya kuweza kumaliza machafuko na pia suluhisho la kisiasa nchini Syria.
"Wajumbe wa nchi hizi hawaonyeshi ishara ya kumaliza machafuko, na kufanyakazi kwa ajili ya kuleta suluhisho nchini Syria".
Hapo kabla balozi wa Ufaransa katika umoja wa mataifa Gerard Araud akiwa kama rais wa baraza la usalama alitangaza kufikishwa mwisho rasmi kwa ujumbe huo wa uchunguzi. Kwa upande mwingine, Araud amesema madhumuni ya kuwapo kwa ujumbe huo hayakufikiwa. Utawala wa Syria pia haukuacha matumizi ya silaha nzito, na machafuko hayajapungua. Mamlaka ya ujumbe huo ambayo yalirefushwa mwezi mmoja uliopita, yanamalizika usiku wa manane siku ya Jumapili. Ilikuwa mwezi Aprili katika baraza la usalama ambapo ujumbe huo ulipewa jukumu la kuzuwia mapigano nchini Syria, lakini jukumu hilo halikutimia, na tangu katikati ya mwezi Juni ujumbe huo umekuwa kwa kiasi kikubwa katika hoteli waliyofikia. Umoja wa mataifa unapaswa kuwapo nchini Syria, lakini kama alivyopendekeza katibu mkuu wa umoja wa mataifa, Ban Ki-moon, hata kama ujumbe huo utaondolewa, lakini ni lazima usaidizi uendelee.
"Tunakubaliana na pendekezo lake la kuanzisha ofisi ya uratibu mjini Damascus".
Anasema hivyo Araud baada ya kikao kilichochukua karibu saa mbili. Utaratibu wa kuwa na uwakilishi mpya wa umoja wa mataifa nchini Syria , utakao kuwa na watu kati ya 20 na 30 , utapata msaada pia kutoka Ujerumani. Kwa mujibu wa mwakilishi wa Ujerumani katika umoja wa mataifa Miguel Berger, ofisi hiyo ya uratibu mbali ya kuwa na watu wa kutosha lakini pia wenye ujuzi unaostahili, ili kuweza kuangalia haki za binadamu.
"Tunaunga mkono , kwa kuwa ni muhimu kuwapo na ushirikiano wa kisiasa , uangalizi wa haki za binadamu, utoaji misaada ya kiutu na ndio sababu kuwapo kwa umoja wa mataifa ni muhimu sana".
Ndio sababu kulikuwa na mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni kutoka mataifa matano yenye kura ya veto katika umoja wa mataifa , China, Ufaransa, Uingereza, Urusi na Marekani, pamoja na wawakilishi kutoka Uturuki, Iraq, Kuwait na Qatar. Mkutano huo wakati huo ulikuwa na lengo la kuunda serikali ya mpito.
Mwandishi: Schmidt, Thomas / ZR / Sekione Kitojo
Mhariri:Josephat Charo