1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria: Mapigano yaendelea Damascus na Aleppo

13 Agosti 2012

Mapigano makali yameripotiwa katika mji mkuu wa Syria Damascus na katika mji wa Aleppo ulio muhimu kibiashara. Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanaarifu kwamba majeshi ya serikali yaliongeza mashambulizi.

https://p.dw.com/p/15ocG
Mapigano yaendelea Damascus
Mapigano yaendelea DamascusPicha: Reuters

Shirika la kutetea haki za binadamu Syria lenye makao yake makuu London, Uingereza, limeeleza kwamba mapigano yalianza Jumatatu alfajiri. Nyumba za raia zilivamiwa na baadhi ya watu wanaoshukiwa kuwa waasi kukamatwa na wapiganaji wa Assad. Mjini Aleppo, jeshi la Assad liliendelea kuwashambulia waasi katika juhudi za kuuteka mji huo ambao ni wa muhimu kabisa kibiashara. Inaelezwa kwamba njia zote za mawasiliano zimekatwa kwenye mji huo. Watu wasiopungua 150 waliuwawa Syria hapo jana.

Kamishna wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Bi Valerie Amos, ametangaza kufanya ziara Syria na Lebanon kufuatia taarifa za kudorora kwa hali ya kibinadamu, jambo linalosababishwa na mgogoro unaoendelea Syria. Amos atafanya ziara yake kuanzia Jumanne hadi Alhamisi ya wiki hii. Akiwa Syria, kamishna huyo anatarajiwa kuzungumzia njia za haraka za kupeleka msaada wa kibinadamu Syria na kupunguza mateso ya raia wa nchi hiyo. Nchini Lebanon, Amos atakutana na wakimbizi kutoka Syria waliokimbia mapigano na atazungumza pia na serikali ya nchi hiyo pamoja na mashirika yanayotoa msaada wa kibinadamu. Inakadiriwa kwamba watu wapatao millioni mbili wameathirika na mgogoro wa Syria hadi sasa.

Nchi za Kiislamu kuijadili Syria

Wakati huo huo, Jumuiya ya ushirikiano wa nchi za Kiislamu imeandaa mkutano juu ya Syria utakaoanza kesho na kufanyika kwenye mji mtakatifu wa Mecca, uliopo Saudi Arabia. Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran, ameelekea Saudi Arabia ambapo ataiwakilisha nchi yake kwenye mkutano huo. Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuanza safari, Ahmadinejad alieleza kwamba serikali za nchi nyingi za Kiislamu zinatumia muda mwingi kujadiliana na akaelezea matumaini yake kwamba mkutano wa kesho utakazia zaidi namna ya kuongezea umoja baina ya nchi hizo na kupunguza hali ya kutokuelewana. Iran, ambayo ni mshirika wa karibu zaidi wa Syria, imeahidi kumuunga mkono Assad katika mapambano yake dhidi ya waasi. Wakati huo huo serikali ya Iran inazishutumu Saudi Arabia, Qatar na Uturuki kwa kuwafadhili waasi.

Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran
Rais Mahmoud Ahmadinejad wa IranPicha: ZDF

Mkutano wa Jumuiya ya nchi za Kiislamu unakuja wakati ambapo Jumuiya ya nchi za Kiarabu imeahirisha mkutano wake uliokuwa pia ufanyike Saudi Arabia. Mkutano huo ulikuwa umelenga kujadili kuhusu mtu wa kuchukua nafasi ya mpatanishi wa Umoja wa Mataifa katika mgogoro wa Syria, Kofi Annan, aliyetangaza kutoendelea na wadhifa huo kufikia mwishoni mwa mwezi huu.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/afp

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman