1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden aupokea mwito wa mazingira wa Putin

23 Aprili 2021

Rais Joe Biden wa Marekani ameeleza kufurahishwa kwake na mwito wa rais wa Urusi Vladimir Putin hii leo wa juhudi za pamoja za kukabiliana na hewa ukaa katika udhibiti wa mabadiliko ya tabia nchi.

https://p.dw.com/p/3sUoh
USA Joe Biden - virtueller Klimagipfel
Picha: Tom Brenner/REUTERS

Rais Joe Biden amesema ana matarajio ya kufanya kazi pamoja na Urusi kuhusiana na masuala ya mazingira. Ameyasema hayo katika siku ya pili ya mkutano wa kilele unaoangazia masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Biden, alipozungumza kwenye mkutano huo uliofanyika kwa njia ya mtandao amesema tayari kumeshuhudiwa hatua kubwa, lakini juhudi zaidi bado zinatakiwa kuchukuliwa na serikali pamoja na sekta binafsi kuhakikisha mabadiliko kuelekea matumizi ya nishati isiyochafua mazingira yanafanyika bila ya kuibua matatizo mengine.

Amenukuliwa akisema iwapo kutafanyika uwekezaji kwenye uthabiti wa kimazingira na miundobinu, kuna uwezekano mkubwa wa kutengeneza fursa kwa kila mmoja.

Prognose: Netanjahus Likud-Partei gewinnt Wahl in Israel
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameahidi kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa ifikapo 2050.Picha: Ronen Zvulun/AP/picture alliance

Awali, waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anayehudhuria mkutano huo hii leo ametoa ahadi ya kupunguza usambazaji wa gesi ukaa hadi ifikapo mwaka 2050, kwa ushirikiano na mataifa mengine ya kikanda katika kufanikisha lengo hilo.

Alisema, "Namshukuru Rais Biden na timu yake kwa kuandaa mkutano huu muhimu. Ninamjua Biden kwa miaka 40. Ninajua uthabiti na kujitolea kwake katika masuala ya mabadiliko ya tabinchi. Hii ni ahadi ambayo sisi Israeli tunashiriki kikamilifu. Ninaahidi kupunguza utoaji wa hewa chafu na kufanikisha mchakato wa mabadiliko kutoka matumizi ya mafuta hadi nishati mbadala ifikapo mwaka 2050."

Mjumbe maalumu wa masuala ya mazingira kutoka nchini Marekani, John Kerry amesema inasikitisha kwamba bado viongozi wengi wanalichukulia suala hili kimzaha na kuongeza kuwa ni mataifa yaliyoathiriwa pakubwa na mabadiliko ya hali ya hewa ndio ambayo yanashinikiza umuhimu wa mkutano wa kilele kuhusu mabadiliko ya tabianchi wa COP26 utakaofanyika Glasgow, Scotland baadae mwaka huu.

Mkutano wa leo umetawalia na masuala ya teknolojia, pamoja na hotuba kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa Bill Gates na Michael Bloomberg baada ya mkutano wa jana kuangazia miito kwa mataifa yanayozalisha kiasi kikuwa cha hewa ukaa kupunguza kiwango hicho ili pia kupunguza ongezeko la joto duniani.

Kenia Uhuru Kenyatta
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ni miongoni mwa viongozi wanaoshiriki mkutano wa kilele wa mazingira ulioitishwa na rais Biden.Picha: imago/i Images

Biden ameitisha mkutano huo wa kilele wa siku mbili na kukutana na wakuu wa mataifa kadhaa kwa lengo la kutangaza kwamba Marekani imerejea kwenye uongozi wa juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi baada ya mtangulizi wake Donald Trumpkujiondoa kwenye makubaliano ya hali ya hewa ya Paris.

Biden aliyeirejesha Marekani kwenye makubaliano hayo jana alitangaza lengo jipya la nchi yake la kupunguza utoaji wa hewa hiyo ya ukaa kutoka asilimia 50 hadi 52 ifikapo mwaka 2030, ikilinganishwa na viwango vya mwaka 2005. Japan na Canada pia zilipandisha viwango vya malengo hayo.

Ikulu ya White House pia iliyahakikishia mataifa mengine kwamba inaweza kufikia lengo hilo, hata kama serikali mpya itaingia madarakani, kwa sababu sekta ya viwanda inaelekea kwenye teknolojia bora zaidi ya nishati safi, magari ya umeme na matumizi zaidi ya nishati mbadala.

Pamoja na wafanyabiashara hao, waziri wa usafirishaji wa Marekani Pete Buttigieg, mwakilishi wa biashara Katherine Tai, waziri wa nishati Jennifer Granholm na waziri wa biashara Gina Raimondo wanatarajiwa kushiriki kwenye mkutano huo.

Viongozi kutoka mataifa ya nje wanaoshiriki mkutano wa leo ni pamoja na rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, waziri mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen, waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu pamoja na rais wa Vietnam Nguyen Xuan Phucare.

Soma Zaidi: Umoja wa Ulaya wafikia makubaliano juu ya tabia nchi kabla ya mkutano wa kilele na rais wa Marekani

Mashirika: RTRE