1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya wafikia makubaliano muhimu juu ya tabia nchi

Zainab Aziz Mhariri: Iddi Ssessanga
21 Aprili 2021

Umoja wa Ulaya umefikia makubaliano ya muda yanayolenga shabaha ya kuondokana kabisa na gesi zinazoharibu mazingira hadi kufikia mwaka 2050 katika nchi zote za jumuiya hiyo.

https://p.dw.com/p/3sKtC
Symbolbild Antarktis
Picha: Mathilde Bellenger/AFP/Getty Images

Serikali na mabunge ya nchi 27 za Umoja wa Ulaya zimekubaliana juu ya malengo mapya ya kudhibiti hewa zinazoharibu mazingira. Nchi za Ulaya zimekubaliana hayo kabla ya kufanyika mkutano kwa njia ya video chini ya uenyekiti wa rais wa Marekani Joe Biden.

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen ameeleza kwamba msimamo wa kisiasa wa nchi za umoja huo  wenye lengo la kuondokana kabisa na hewa chafu, hadi kufikia mwaka 2050 umo katika msingi wa kisheria. Sheria juu ya tabia nchi inauweka Umoja wa Ulaya kwenye njia ya mazingira bora kwa muda wa miaka 30.

Kulingana na makubaliano ya muda yaliyofikiwa nchi hizo za Umoja wa Ulaya pia zitajizatiti kufikia haraka, lengo la kupunguza utoaji wa gesi chafu kwa asilimia 55 mpaka utakapofika mwaka 2030, kulinganisha na viwango vya mwaka wa 1990.

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen
Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der LeyenPicha: Olivier Hoslet/REUTERS

Mbunge wa Ulaya Peter Liese anayeiwakilisha kambi ya wabunge wa EPP Christian Democratic, amesema wakati umefika wa makubaliano kama hayo kwa sababu bara la Ulaya linapaswa kuonyesha msimamo wake katika muktadha wa hatua chanya zilizochukuliwa na China pamoja na Marekani.

Lengo la hapo awali lilikuwa kupunguza utoaji gesi zinazoharibu mazingira kwa asilimia 40 hadi kufikia mwaka wa 2030. Hata hivyo kutokana na shinikizo linalotokana na ushahidi dhahiri wa kuzidi kuharibika kwa mazingira na pia kutokana na wananchi kujenga mwamko mkubwa zaidi juu ya mazingira, lengo hilo limewekwa kuwa la juu zaidi.

Wabunge wa kambi ya Kijani walalamika

Wabunge wa kambi ya kijani kwenye bunge la Ulaya wamelalamika kwamba njama kadhaa zimetumika ili kufikia lengo la asilimia 55. Mtaalamu wa masuala ya mazingira wa kambi hiyo ambaye ni mbunge wa Ulaya bwana Michael Bloss amesema nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zimeharakisha kuipitisha sheria hiyo dhaifu juu ya tabia nchi ili kuweza kusimama na kupiga picha pamoja na rais wa Marekani Joe Biden.

Mwenyekiti wa mazungumzo, Pascal Canfin kutoka kambi ya Waliberali ameshauri itafutwe njia ya kuwaleta wajumbe wote pamoja. Hata hivyo amesisitiza kwamba mwafaka uliofikiwa utaziwezesha nchi za Ulaya kutimiza mengi zaidi mnamo kipindi cha miaka 9 ijayo na kuvuka yale yaliyofanyika katika miaka 10 iliyopita. Makubaliano hayo ya nchi za Umoja wa Ulaya bado yanapaswa kuidhinishwa rasmi na nchi zote wanachama  japo hiyo itakuwa kama hatua ya rasimu tu.

Rais wa Marekani Joe Biden
Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Evan Vucci/AP/picture alliance

Marekani ambayo ni mharibifu mkubwa kabisa wa mazingira ikifuatiwa na China, inajitayajirisha kutangaza malengo yale mapya juu ya kupunguza utoaji wa gesi chafu. Chini ya urais wa Joe Biden, Marekani imerejea kwenye mkataba wa Paris wa mwaka 2015 juu ya mazingira.

China pia inakusudia kutangaza malengo yake mapya juu ya hatua za kupunguza gesi zinazoharibu mazingira hadi kufikia mwaka 2030.Nao Umoja wa Ulaya umesema utasimama mstari wa mbele kwa uamuzi wake baada ya Marekani kuyafafanua malengo yake.

Umoja wa Ulaya na Marekani zote zinaazimia kuondokana na uzalishaji wa hewa ya kaboni hadi kufikia katikati mwa karne hii hatua ambayo wataalamu wanasema ili kufikia lengo hilo la kuondokana kabisa na gesi ya kaboni itabidi kuzuia joto kupanda na kuvuka nyuzi joto 2 kwa wastani hadi kufikia mwaka 2100.

Chanzo: AP