Assange kufunguliwa upya mashitaka ya ubakaji
13 Mei 2019Hatua hiyo inaleta mapambano ya kisheria na Marekani, ambako mdukuzi huyo raia wa Australia anatakiwa kwa kudukua kompyuta za wizara ya mambo ya ndani Pentagon. Mamlaka za Uingereza zitaamua ikiwa ombi hilo la kumrejesha Assange litakubaliwa.
Assange alitafuta hifadhi kwenye ubalozi wa Equador jijini London mwaka 2012 ili kuepuka kupelekwa nchini Sweden kwa ajili ya kuhojiwa. Mwezi uliopita aliondolewa ubalozini baada ya kukiuka masharti ya hifadhi. Alikamatwa na polisi wa Uingereza Aprili 11 na kwa hivi yuko jela ya Bermarsh akitumikia kifungo cha wiki 50 kwa kukiuka dhamana mwaka 2012.
Eva-Marie Persson, ambaye ni naibu mkurugenzi wa waendesha mashitaka wa umma, aliviambia vyombo vya habari siku ya Jumatatau kuwa "kuna kila nia ya kushuku kwamba Assange alifanya ubakaji". Soma zaidi...
Waendesha mashitaka wa Sweden walifungua mashitaka ya awali, lakini hatua hiyo ilishindwa kufikia mashitaka rasmi dhidi ya Assange baada ya kuitembelea nchi hiyo mwaka 2010, kufuatia malalamiko kutoka kwa wanawake wawili wa Sweden ambao walidai kuwa wahanga wa unyanyasaji wa kingono uliofanywa na Assange.
Wakati mashitaka hayo ya unyanyasaji kingono yakifutwa mwaka 2017 kufuatia kumalizika kwa kipindi cha kusikilizwa kesi, madai ya ubakaji bado yamesalia. Mamlaka za Sweden zilishindwa kuyafuatilia kwasababu Assange alikuwa akiishi ubalozini na hapakuwa na mwelekeo wa kupelekwa nchini humo.
Assange amekana kutenda uhalifu huo, akisema madai hayo yamechochewa kisiasa. Mwanzilishi huyo sasa anatakiwa kuhojiwa nchini Sweden, huku pia akitakiwa Marekani kwa kula njama na Chelsea Manning aliyekuwa mwanajeshi wa Marekani kwa kudukua kompyuta za Pentagon.
Wakili anayemtetea Assange Per E. Samuelson alisema kuyafungua tena mashitaka ya ubakaji ni "fedheha". "Yuko jela Uingereza na anakabiliwa na kitisho cha kupelekwa Marekani", alisema wakili huyo.
Lakini wakili wa mwanamke aliyeripoti kubakwa na Assange ana matumaini baada ya kesi kufunguliwa tena kwa mujibu wa Wakili wake Elisabeth Massi Fritz.
Assange anakabiliwa na kifungo cha miaka minne jela nchini Sweden ikiwa atakutwa na hatia. Inaweza kuchukua mwaka au zaidi hadi kibali cha kupelekwa Marekani au Sweden kukubaliwa.