1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano kudai muasisi wa WikiLeaks Assange aachiliwe

Oumilkheir Hamidou
12 Aprili 2019

Katika wakati ambapo Australia inasema itapinga adhabu ya kifo kwa Julian Assange pindi akipelekwa Marekani , maelfu wanateremka majiani mijini Sydney na Melbourne kudai muasisi huyo wa WikiLeaks aachiwe huru

https://p.dw.com/p/3GfYk
England Protest Unterstützer Julian Assange
Picha: picture-alliance/empics/V. Jones

 

Julian Assange,  raia wa Australia  aliyeanzisha mtandao wa WikiLeaks alikamatwa akiwa katika ubalozi wa Equador mjini London na jaji kumkuta na hatia  ya kuvunja masharti ya dhamana. Anakabiliwa na mashitaka nchini Marekani ya kufichua siri za seikali.

Waziri Mkuu wa Australia Scott Morrison amesema  nchi yake haihusiki hata kidogo na mipango ya kumpeleka Marekani na kwamba Assange atapatiwa huduma za kawaida na maafisa wa ubalozi mdogo wa Australia.

Kwa upande wake, waziri wa mambo ya nchi za nje Marise Payne akijibu hofu za mashabiki wa Assange kuhusu uwezekano wa adhabu atakayopewa nchini Marekani, amesema Australia inapinga moja kwa moja adhabu ya kifo". Ameongeza kusema Uingereza imetaka ihakikishiwe na Marekani kwamba Assange hatohukumiwa adhabu ya kifo pindi akipelekwa nchini humo.

Maandamano mjini London kudai Assange aachiwe huru
Maandamano mjini London kudai Assange aachiwe huruPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Dunham

Maandamano mijini Sydney na melbourne kudai Assange aachiwe huru

Harakati za kumuunga mkono Assanze zimeanza katika nchi alikozaliwa Australia. Watu wasiopungua 30 waliandamana katika eneo la kati ya Sydney baada ya kukusanyika nje ya ubalozi mdogo wa Uingereza na kutoa wito aachiliwe huru yule wanaemtaja kuwa "mshika bendera wa wanaopigania ukweli na uhuru wa mtu kuzungumza.

Wakibeba maaandishi yanayosema "Aachiwe huru Assange. Asipelekwe Marekani,"waandamanaji hao wanapaza pia sauti wakidai Assange "Msema kweli aachiwe huru na mjumbe asipigwe risasi". Kundi jengine dogo la watu wameandamana katika mji wa Melbourne pia.

Julian Assange alipokamatwa na kufikishwa mahakamani mjini London
Julian Assange alipokamatwa na kufikishwa mahakamani mjini LondonPicha: picture-alliance/ZUMAPRESS/R. Pinney

Assange anandamwa kwaajili ya shughuli zake kama mwandishi habari

Shirika la waandishi habari wa Australia, muungano wa mashirika ya vyombo vya habari na sanaa nayo pia yanaunga mkono Assange aachiliwe huru. Mwenyekiti wa shirika hilo, Marcus Strom anasema Assange anaandamwa kwa sababu ya shughuli zake kama mwandishi habari. Akikumbusha kwamba mwaka 2011 WikiLeaks walitunukiwa tuzo muhimu kabisa ya uandishi ya Australia, Strom amesema kadhia ya Assange inahusiana na uhuru wa vyombo vya habari.

"Julian Assange anaandamwa kwasababu ya shughuli za uandishi zilizoendeshwa na WikiLeaks na shughuli hizo zinahusiana  na kufichua habari ambazo ni za maslaha bayana kwa jamii kuhusu visa vya kikatili, na  pengine uhalifu wa kivita uliofanyika Iraq na Afghanistan" amesema mwenyekiti wa shirika la waandishi habari nchini Australia, Marcus Strom.

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AP

Mhariri: Mohammed Khelef