1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muasisi wa WikiLeaks Julian Assange akamatwa London

11 Aprili 2019

Muasisi wa mtandao wa WikiLeaks, Julian Assange, leo ametolewa kwa nguvu kutoka ubalozi wa Ecuador jijini London na kutiwa kwenye karandiga ya polisi ya Uingereza.

https://p.dw.com/p/3GcqQ
Großbritannien London - Julian Assange festgenommen
Picha: Reuters/P. Nicholls

Polisi wa Uingereza wamemtia mbaroni Assange kutokana na waranti wa mahakama wa tangu mwaka wa 2012, baada ya Ecuador, taifa la Amerika Kusini, kuamua kufuta kibali cha uhamiaji kutokana na sababu za kisiasa, ambacho kilimpa Assange ulinzi wa kutokamatwa kwa kipindi cha karibu miaka saba. Katika taarifa polisi imesema Assange anazuiliwa katika kituo kimoja cha polisi katikati mwa London mpaka atakapopandishwa kizimbani katika mahakama ya Westminster haraka itakavyowezekana.

Rais wa Ecuador, Lenin Morero, amesema nchi yake imezingatia haki za uhuru wake wakati ilipoamua kufuta kibali cha uhamiaji cha muanzilishi wa mtandao wa WikiLeaks, Julian Assange. "Tabia isiyostahiki na ya fujo ya Julian Assange, matangazo ya chuki na vitisho ya shirika lake dhidi ya Ecuador, pamoja na kutoheshimu mikataba ya kimataifa, kumeifanya hali kufikia wakati ambapo kibali cha uhamiaji cha Assange si halali. Ecuador imeamua kufuta hifadhi ya kidiplomasia aliyopewa Assange mwaka 2012."

Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Uingereza, Jeremy Hunt, ameishukuru serikali ya Ecuador kwa ushirikiano wake katika kukamatwa Assange, akiandika katika mtandao wake wa twitter kwamba Assange si shujaa. "Tulichokiona leo ni kwamba hakuna aliye juu ya sheria. Julian Assange si shujaa. Amejificha kuepuka ukweli kwa miaka na miaka na ni kweli mustakbali wake unapaswa kuamuliwa na mfumo wa sheria wa Uingereza. Hatumhukumu yoyote kama ana hatia ama la. Hilo mahakama itaamua, lakini kisichokubalika ni mtu kuukwepa mkono wa sheria na amekuwa akifanya hivyo kwa muda mrefu. Ndio maana yeye si shujaa."

Marekani yamfungulia mashitaka Assange

Assange alijificha katika ubalozi wa Ecuador jijini London mnamo mwaka 2012 baada ya kuachiwa kwa dhamana nchini Uingereza alipokabiliwa na kitisho cha kurejeshwa  Sweden kutokana na madai ya unyanyasaji wa kingono, ambayo yalifutiliwa mbali. Lakini wakili wa mwanamke wa Sweden aliyemtuhumu Assange kwa kumbaka mwaka 2010 amesema yeye na mteja wake watawaomba waendesha mashitaka wa Sweden waufungue tena uchunguzi uliofutwa mwaka 2017.

London Botschaft Ecuador Protest nach Festnahme von Julian Assange
Shabiki wa Assange, Kyle Ferran, akiandamana nje ya ubalozi wa Ecuador jijini LondonPicha: picture-alliance/empics/J. Stillwell

Waendesha mashitaka wa Marekahi wamesema leo wamemfungulia mashitaka Assange ya kula njama kwa kujaribu kufanya udukuzi katika kompyuta moja ya serikali ya Marekani iliyokuwa na mchambuzi wa masuala ya kijasusi wa jeshi la Marekani, Chelsea Manning, mwaka 2010. Wizara ya sheria ya Marekani imesema katika taarifa kuwa Assange anakabiliwa na adhabu kali kabisa ya kifungo cha miaka mitano jela.

Wakati haya yakiarifiwa, Dmitry Peskov, msemaji wa rais wa Urusi, Vladimir Putin, ameelezea matumaini yake kwamba maafisa wa Uingereza wataziheshimu haki za Assange baada ya kumtia ndani. Urusi imempa hifadhi mwanaharakati mwingine wa kupigania uwazi katika utendaji wa serikali, mtaalamu wa kompyuta wa Marekani na wakala wa zamani wa shirika la usalama wa taifa NSA, Edward Snowden. Mtandao wa WikiLeaks ulimsaidia Snowden kukimbia kutoka Hong Kong hadi mjini Moscow nchini Urusi mwaka 2013. Snowden amesema wakosoaji wa Assange huenda wakafurahia, lakini huu ni wakati mgumu kwa uhuru wa vyombo vya habari.

afpe, dpae, reuters,ap