1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al-Shabbaab yaapa kukabiliana na wanajeshi wa Kenya nchini Somalia

17 Oktoba 2011

Wanamgambo wa Al-Shabaab nchini Somalia wameahidi kulipiza kisasi dhidi ya wanajeshi wa Kenya walioingia katika ardhi ya Somalia kwa lengo la kuwatafuta raia wanne wa Ulaya waliotekwa nyara wiki iliyopita.

https://p.dw.com/p/RrJk
Jeshi la Kenya katika mazoezi ya kawaida kwenye uwanja wa Uhuru nchini Kenya.
Jeshi la Kenya katika mazoezi ya kawaida kwenye uwanja wa Uhuru nchini Kenya.Picha: dapd

Wanajeshi wa Kenya walivuuka mpaka na kuingia katika ardhi ya Somalia kiasi kilomita 100 kutoka eneo la mpaka wa kaskazini mwa Kenya hapo jana (16.10.2011), wakisaidiwa na helikopta.

Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya mawaziri wawili wa Kenya kusema kwamba wanamgambo hao wa al Shabaab wanahusika na utekaji nyara wa raia hao wa kigeni tukio lililofanyika katika ardhi ya Kenya. Kenya imewatangaza wapiganaji wa kundi la Al-Shabbaab kuwa maadui zao.

Hii leo afisa wa ngazi ya juu wa kundi hilo la kiislamu lenye siasa kali nchini Somalia, Sheikh Hassan Turki, amewatolea mwito wapiganaji wote wa makundi ya siasa kali pamoja na waislamu kujitokeza kutetea nchi hiyo ya Somalia dhidi ya kile alichokiita wanajeshi maadui.

Aidha afisa huyo ametoa ahadi kwamba wanajeshi wa Kenya watasukumwa nyuma na kurudishwa kwao.

Wasiwasi mkubwa umetanda nchini Kenya kwamba wapiganaji wa kundi hilo huenda wakalipiza kisasi kutokana na hatua ya jeshi la Kenya kuingia katika ardhi ya Somalia.

Wanamgambo wa Al Shabaab wanaofungamanishwa na kundi la kigaidi la Al Qaeda walifurushwa kutoka mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, mnamo mwezi Agosti mwaka huu na pia wamekuwa wakikabiliwa na hali ngumu katika mapambano ya hivi karibuni na vikosi vya serikali vinavyosaidiwa na Umoja wa Afrika.

Kundi hilo pia hivi karibuni lilifanya shambulio baya kabisa la kujitoa muhanga lililosababisha vifo vya watu 70 katika mji wa Mogadishu huku wachambuzi wa mambo wakionya kwamba huenda kundi hilo likafanya mashambulio zaidi siku zijazo.

Mwandishi: Saumu Mwasimba/DPA
Mhariri: Josepht Charo