Zoezi la kuhesabu kura laendelea Mali
30 Julai 2018Zoezi hilo la kuhesabu kura lilianza mjini Bamako baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa saa kumi na mbili jioni hapo jana. Katika shule moja ya msingi iliotumiwa kama kituo cha kupigia kura maafisa walijumuisha matokeo katika ubao wa kuandikia.
Hata hivyo matokeo rasmi bado hajayatolewa na wagombea wamezuiwa kutangaza chochote kabla ya matokeo rasmi kutangazwa. Watu milioni 8 ndio walioandikishwa kupiga kura na wagombea katika uchaguzi huu wanajumuisha wafanyabiashara, mwanasayansi na mwanamke mmoja.
Wagombea hao zaidi ya 20 wanapigania nafasi ya urais katika taifa kubwa lililo eneo la Jangwa la Sahara lililoharibiwa na waasi wa kituareg na mashambulizi ya wanamgambo wa kiislamu katika maeneo yake ya Kaskazini na maeneo ya kati tangu kulipofanyika uchaguzi uliopita mwaka 2013.
Katika maeneo mengine ya Mali, uchaguzi haukufanyika kutokana na ukosefu wa usalama huku Mkuu wa Ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Ulaya Cecile Kyenge ameihimiza serikali nchini humo kuweka wazi maeneo ambayo uchaguzi haukufanyika ili kuwaondolea wasiwasi wagombea.
Ukosefu wa usalama wazuia zoezi la uchaguzi kufanyika katika baadhi ya maeneo Mali
Katika mkutano na waandishi habari hapo jana jioni, Mkurugenzi wa kampeni ya mgombea Soumaila Cisse, mwenye umri wa miaka 68 ambaye ndie mshindani wa karibu wa rais Keita, amekadiria kuwa vituo vya kupigia kura 644 kati ya 23,000 havikuweza kufunguliwa wakati wa zoezi la uchaguzi kutokana na ukosefu huo wa usalama.
kilomita 1000 kutoka Kusini Magharibi mwa mji wa Bamako Hama Diallo aliye na miaka 32 anasema matumaini yake ni kuona siku za usoni zilizo salama. Ameongeza kuwa anatumai rais atakaechaguliwa ataweka kipaumbele katika masuala ya Usalama.
Miaka mitatu iliyopita mashambulizi ya wapiganaji wa jihadi yamezidi nchini Mali na kuongeza mara mbili vifo vitokanavyo na vurugu hii ikiwa ni kulingana na tovuti ya shirika la kiraia Malilink.
Wanamgambo wamesambaa kutoka Kaskazini hadi maeneo ya kati na kulenga mji mkuu Bamako wakati watu waliojihami kwa bunduki waliposababisha vifo vya watu 20 wapovamia hoteli moja mwaka 2015.
Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters
Mhariri:Yusuf Saumu