Sheria ya kupiga marufuku kanisa la Orthodox yapita Ukraine
24 Agosti 2024Zelensky aliidhinisha muswada huo uliokosolewa na Urusi kwenye siku ya uhuru wa taifa hilo kutoka katika muungano wa kisovieti na miaka miwili na nusu tangu Moscow ilipoanzisha uvamizi wake nchini humo.
Katika hotuba yake Zelensky pia alisema Urusi inataka kuiharibu kabisa Ukraine lakini kwa sasa vita vimerejea nchini humo, akimaanisha mashambulizi yanayofanywa na jeshi lake katika eneo la Kursk aliyosema yanalenga, kuizuwia Urusi kuendelea kuishambulia huku Urusi nayo ikisonga mbele kuendelea kutaka kudhibiti miji zaidi ya Ukraine.
Urusi imesema majeshi yake yameiteka sehemu kubwa ya jimbo la Donetsk.
Kwengineko Urusi kupitia gavana wa jimbo la Voronezh Alexander Gusev, imetangaza hali ya dharura katika sehemu ya jimbo hilo linalopakana na Ukraine, baada ya shambulizi la droni lililofanyika usiku kucha. Gusev amesema wamefanikiwa kudungua droni tatu, hakuna aliyejeruhiwa na wamefanikiwa pia kuwahamisha watu takriban 200 kutoka katika eneo hilo linalodaiwa kushambuliwa na Ukraine.