Yuko wapi Azory Gwanda?
21 Novemba 2019Mwandishi huyo ambaye alikuwa akifichua taarifa za mauji ya raia yaliyokuwa yakifanyika katika eneo la Kibiti Mkoani Pwani, anaingia katika kumbukumbu ya dunia kwa kuwa mwandishi wa habari wa kwanza nchini Tanzania kutoweka katika mazingira ya kutatanisha.
Licha ya jitihada zilizofanywa na waandishi wa habari, mashirika ya kiraia na jumuiya ya kimataifa, kitendawili cha hatma yake bado kimeendelea kutatiza tasnia ya habari na hivyo kuibua hali ya wasiwasi miongoni mwao.
Kutimia miaka miwili bila kujua hatma ya mwanahabari huyo ni mtihani unaokosa majibu ya moja kwa moja. Ingawa wanahabari nchini wamekuwa wakipitia madhila ya aina nyingi, tukio hili likiwa limewaogopesha wengi.
Ujasiri wa kuandika habari za uchunguzi, kuripoti na kuchambua masuala tete yanayohusu taifa ni mambo ambayo sasa yanafanywa kwa uangalifu mkubwa. Wengi wa wanahabari wanasita kujikita katika masuala ya namna hiyo wakihofia pengine yanaweza kuwakuta kama yale yaliyomkuta Azory.
Bado hapajakuwa na taarifa za matumaini kuhusu kupotea kwake
Maisha ya Azory na kutoweka kwake, kumeacha alama ambayo waandishi wa habari daima watakumbuka na hata wakati mwingine itawapasa kuchunga kalamu zao. Nyakati hizi ambazo kumekuwa na sheria zinazodaiwa kubinya uhuru wa habari, ni changamoto nyingine ambayo inafanya tasnia hii ionekane ni moja kati ya taaluma za hatari nchini Tanzania.
Hata hivyo, pamoja na hali ya wasiwasi inayoendelea kuwaandama waandishi wa habari, mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Deudatus Balile anasema waandishi wa habari hawapaswi kukataa tamaa, akitaka waendelee na juhudi za kumsaka.
Azory Gwanda anaaminika kuchukuliwa na watu wasiojulikana wakati akiendelea kuripoti matukio ya watu kuuawawa katika Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani. Mara kadhaa serikali imekuwa ikisema inaendelea kufuatilia juu ya kutoweka kwake ingawa hadi sasa hakuna taarifa zozote za matumaini.
Tangu atoweke matamko kadhaa yamekuwa yakitolewa ikiwamo Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari(CPJ) ambayo hutoa mwito ikiitaka serikali kulipa umuhimu suala hilo.
Mitandao ya kijamii imekuwa jukwaa lingine linalotumiwa na wanaharakati kupaza sauti kuhusiana na kutoweka kwake.
Mapema mwezi Mei mwaka huu jina la Azory lilijitokeza katika orodha ya matukio 10 muhimu duniani yaliyohusu waandishi wa habari.
Chanzo: George Njogopa Tanzania