Yemen: Wahouthi washambuliwa tena
23 Aprili 2015Waziri wa ulinzi wa Marekani Ash Carter amesema nchi yake inatiwa wasiwasi mkubwa na mzigo zinaoubeba meli za mizigo za Iran, na kuionya nchi hiyo kuacha kuchochea mzozo uliopo kwa kupeleka silaha zaidi. Hayo waziri Carter aliyasema mbele ya kundi la waandishi wa habari akiwa njia kuelekea jimboni California.
Rais wa Marekani Barack Obama alisema Jumanne wiki hii, kwamba tayari nchi yake imeionya Iran dhidi ya kuwapa waasi wa kihouthi silaha ambazo zinaweza kutishia meli zinazopita katika Ghuba ya Eden.
Ash Carter amesema meli za kivita za Marekani ambazo zimepelekwa karibu na pwani ya Yemen, zina lengo la kumpa rais Obama uwezo wa kuchukua hatua, lakini amesita kusema iwapo ikibidi wamarekani wanaweza kuingia katika meli hizo za Iran.
''Sitawaambia kile ambacho Marekani iko tayari kukifanya, lakini kama alivyosema rais, tuna njia zaidi ya moja'' ametangaza wari wa ulinzi wa Marekani mbele ya waandishi wa habari.
Mashambulizi mapya yalenga ngome za wahouthi
Huku Marekani ikihofu juu ya shehena inayobebwa na meli za Iran, nchini Yemen kwenyewe mashambulizi mapya ya Saudi Arabia na washirika wake yameendelea leo. Mashambulizi hayo yalianza upya jana, saa chache tu baada ya muungano huo unaoongozwa na Saudi Arabia kutangaza mwisho wa operesheni yake ya anga dhidi ya wahouthi, ambayo ilikuwa imedumu kwa takribani mwezi mzima.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ambaye mara kwa mara ametoa wito wa kusitishwa mapigano nchini Yemen, amesema amesikitishwa na kuanza upya kwa mapigano hayo, na kuongeza kuwa anayo imani kwamba yatasitishwa haraka iwezekanavyo.
Takwimu mpya za shirika la afya ulimwenguni zinaonyesha kuwa idadi ya watu waliouwa katika vita vya Yemen tangu tarehe 19 Machi hadi mwanzoni mwa wiki hii imefika 1,080.
Rai ya mazungumzo ya kisiasa
Msemaji wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu katika eneo la Mashariki ya Kati Robert Mardini ametoa rai ya suluhu kwa mzozo huo.
''Mzozo wa Yemen unahitaji haraka suluhisho la kisiasa, lakini kwa wakati huu hali ya kibinadamu inazidi kuzorota siku baada ya siku. Tunaziomba pande zote kuwalinda wanawake, wanaume na watoto, na tunataka ziruhusu upelekaji wa msaada wa kiutu''. Amesema msemaji huyo.
Shirika la msalaba mwekundi vile vile limesema kwamba mamia ya watu wamekamatwa na kuwekwa kizuizini nchini Yemen. Wanaharakati wa upinzani nchini humo, wamesema kwamba waasi wa kihouthi wanawakamata watu wote wanaopinga mamlaka yao katika miji ya Sanaa, Taiz na maeneo mengine.
Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre/dpae
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman