1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yajjimarisha Ghuba ya Arabuni

21 Aprili 2015

Marekani imethibitisha inazifuatilia meli za Iran zinazoshukiwa kuwa zimechukuwa silaha kuwapelekea waasi wa Kihouthi nchini Yemen wakati ikiimarisha uwepo wake kijeshi katika Bahari ya Arabuni.

https://p.dw.com/p/1FBeF
Meli ya kivita ya Marekani USS Theodore Roosevelt.
Meli ya kivita ya Marekani USS Theodore Roosevelt.Picha: Kitwood/Getty Images

Jeshi la majini la Marekani limepeleka meli yake ya kivita ya USS Theodore Roosevelt ikisindikizwa na meli yenye kubeba makombora ya USS Normandy kuhakikisha kile ilichosema njia muhimu za bahari katika eneo hilo zinabakia kuwa wazi na salama na kufanya idadi ya meli za kivita za Marekani katika eneo hili kufikia tisa.

Kwa mujibu wa afisa mwandamizi wa ulinzi wa Marekani ambaye amezungumza na shirika la habari la Ufaransa AFP msafara wa meli za Iran unajumuisha meli tisa zikiwemo mashua mbili za doria lakini mahala hasa unakoelekea msafara huo hakujulikani.

Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani Kanali Steven Warren amekanusha repoti kwamba meli za Marekani zimeagizwa kuzuwiya meli za Iran zenye kuwapelekea silaha Wahouthi.

Meli za Iran yumkini zikazuiliwa

Marekani imesema haishiriki moja kwa moja katika mashambulizi ya anga ya ushirika unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya waasi wa Kishia wa jamii ya Wahouthi nchini Yemen lakini inasaidia kwa kutowa taarifa za kijasusi na msaada wa vifaa.

Manowari ya Iran.
Manowari ya Iran.Picha: picture-alliance/dpa

Maafisa kadhaa wa serikali ya Marekani wamedokeza kwamba yumkini Saudi Arabia,Misri na washirika wao wengine ndio zitazozizuwiya meli hizo za Iran itakapolazimika.

Inasemekana kwamba msafara huo wa meli za Iran tayari umevuka mlango bahari wa Hormuz kuondoka Ghuba na hivi sasa unaelekea upande wa magharibi ambapo inaaminika kuwa Yemen.

Upatanishi wa Iran wagonga ukuta

Rais Hassan Rouhani wa Iran leo ametowa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano nchini Yemen na kukomeshwa kwa mashambulizi ya anga ya ushirika unaongozwa na Saudi Arabia ili kuwezesha kufanyika kwa mazungumzo kati ya pande zinazohasimiana nchini humo.

Rais Hassan Rouhani wa Iran.
Rais Hassan Rouhani wa Iran.Picha: picture-alliance/epa/A. Taherkenareh

Rais Rouhani amesema"Tunataraji kwamba kila mtu atazinduka na tunatumai pendekezo la Iran litatekelezwa.Ni kusitishwa kwa mapigano mara moja,kushughulikia hali ya majeruhi na kufanya mkutano baina ya Wayemen kutafuta suluhisho na hatimae kuunda serikali yenye kushirikisha makundi na makabila yote.Tunaamini kwamba huu ni ufumbuzi ambao unaweza kutatuwa masahibu ya Yemen."

Rais Rouhani ametowa kauli hiyo muda fupi kabla ya kuondoka katika uwanja wa ndege wa Mehrabad mjini Tehran kuelekea Indonesia kuhudhuria mkutano wa Kilele wa Asia na Afrika.

Dhima ya Iran

Unyeti wa dhima ya Iran katika mzozo huo umezidi kujitokeza leo hii wakati serikali ya Yemen ilipokataa pendekezo la Iran la kusuluhisha mzozo huo.Waziri wa mambo ya je wa Yemen Riyadh Yassin amesema juhudi zozote zile za upatanishi kutoka Iran hazikubaliki kwa sababu Iran inahusika katika mzozo huo wa Yemen.

Moshi mzito ukifuka baada ya shambulio la ghala la silaha Sanaa. (20.04.2015)
Moshi mzito ukifuka baada ya shambulio la ghala la silaha Sanaa. (20.04.2015)Picha: Reuters/Khaled Abdullah

Amesema Wahouthi na vikosi vya Rais wa zamani Ali Abdullah Saleh lazima waondoke katika miji na vijiji vyote vya Yemen ikiwemo Sanaa na Aden na kurudi katika ngome yao kuu ya kaskazini ya mji wa Saada wakiwa kama raia na kusalimisha silaha zao.

Nchini Yemen kwenyewe mzozo huo hauonyeshi dalili ya kupowa wakati idadi ya vifo vya raia waliouwawa katika mashambulizi ya anga yanayongozwa na Saudi Arabia dhidi ya ghala la makombora mjini Sanaa hapo jana ikiongezeka na kufikia 38 huku watu 532 wakiwa wamejeruhiwa.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman